
| CUF wamng’ang’ania Raza | Send to a friend |
| Saturday, 28 January 2012 09:06 |
|
MGOMBEA wa Chama Cha Wananchi (CUF) katika uchaguzi mdogo wa kiti cha uwakilishi wa Jimbo la Uzini, mjini Zanzibar, Salma Husein Zarali, amekata rufaa katika Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kupinga uamuzi uliotolewa na ofisi tume hiyo katika Wilaya ya Kati Unguja, kuhusu mgombea wa CCM, Mohamed Raza. Mgombea huyo wa CUF alikuwa amewasilisha katika ofisi hiyo, pingamizi la kutaka Raza aondolewe katika kinyang’anyiro hicho kwa madai kuwa amekosa sifa za kumwezesha kugombea. Salma alitoa msimamo huo jana, alipokuwa akizungumza na mwandishi wa habari hii, huko Uzini.Mgombea huyo wa CUF alisisitiza kuwa Raza amevunja sheria ya uchaguzi namba 46 kifungu kidogo 3 (a) na kuitaka tume itumie kifungu cha 44 (4) kumwengua. Alidai kuwa mgombea yeyote wa nafasi ya uwakilishi wa jimbo, anapaswa kula kiapo mbele ya hakimu wa mkoa, lakini Raza amekula kiapo chake mbele ya hakimu wa wilaya. “Sisi tunaenda mbele zaidi kudai haki yetu ya msingi dhidi ya mgombea huyu ambaye kimsingi hastahiki kugombea kwa kuwa amekiuka sheria,” alisema Salma. Jana ofisi ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar katika Wilaya ya Kati ilitupilia mbali pingamizi zilizowasilishwa na CUF na Chadema dhidi ya Raza, kwa maelezo kwamba kisheria madai yao hayana msingi. Lakini Salma alisema kama tume itaendelea kumbeba Raza, wao watakwenda mahakamani kuomba uchaguzi usitishwe hadi hapo sheria zitakapofuatwa.“ Kama wakiendekleza na msimamo wa wao, sisi tutakwenda kudai haki mahakamani,” alisema. |













