|
Raymond Kaminyoge WAKATI kipenga cha uchaguzi katika Jumuiya za Chama cha Mapinduzi (CCM) kikipulizwa leo kwa wanachama kuanza kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali, viongozi wa jumuiya za chama hicho wameonya kuwa watakaojihusisha na rushwa watakiona cha mtema kuni.
Viongozi hao wamesema wako makini katika kudhibiti vitendo vya rushwa na kuwaonya wanachama wa jumuiya hizo kutojihusisha kabisa na vitendo vya rushwa. Kauli hizo zilitolewa jana kwa nyakati tofauti na Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sophia Simba na Katibu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) Martin Shigella. Kauli hizo za viongozi wa Jumuiya za CCM, zimekuja baada ya kutolewa kwa ratiba ya kuanza kwa uchukuaji fomu za kugombea uongozi wa ngazi mbalimbali za chama hicho. Akizungumzia zoezi hilo, Simba alisema alikutana na makatibu wa mikoa na wilaya wa UWT ili kupanga namna ya kudhibiti vitendo vya rushwa ili uchaguzi uwe huru na haki.
“Tumekutana na kufundana kuhusu vitendo vya rushwa, natoa wito kwa wanawake waache kujihusisha na rushwa atakayethubutu atakiona cha mtema kuni,” alisema Simba ambaye pia ni Waziri Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto. Simba aliwashauri wanawake ambao ni wanachama wa jumuiya hiyo kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali. “Nawaomba wasimamizi wa mchakato huu wa uchaguzi kuwa wawazi kwa wanachama ili uchaguzi uwe huru na haki ili kuepukana na vitendo vya rushwa,” alisema Simba.
Katibu wa UVCCM, Shigela alionya matumizi ya fedha katika mchakato wa uchaguzi huo na kuwataka wanachama wa jumuiya hiyo kujiepusha na vitendo vya rushwa. Alisema umoja huo hautawaonea aibu wanachama watakaojihusisha na rushwa katika mchakato huo wa uchaguzi.
Alisema vikao vya watendaji wa umoja huo vimekwishafanyika ili kukumbusha namna ya kufuata maadili katika uchaguzi huo. Shigela aliwashauri vijana wanachama wa umoja huo kujitokeza kwa wingi kuchukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali. Katibu wa itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema asingependa kusema chochote sasa kwa kuwa uchaguzi huo unaanza na jumuiya.
"Ni kweli kuna mikakati mingi ya uchaguzi huo lakini mimi nakushauri leo (jana) uwatafute viongozi wa jumuiya wakueleze walivyojipanga kwa kuwa uchuguzi unaanza kwenye ngazi za jumuiya," alisema. Ratiba iliyotolewa na chama hicho mapema mwezi uliopita imeonyesha kuwa uchaguzi huo umegawanyika katika sehemu kuu mbili; uchaguzi wa viongozi wa chama na uchaguzi wa jumuiya.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo, wanachama watakaowania uongozi kwenye jumuiya katika ngazi ya shina, wataanza kuchukua fomu kuanzia leo Februari 4 na uchaguzi utafanyika Februari 29, mwaka huu. Kwa upande wa uongozi wa chama ngazi hiyo ya shina, uchukuaji fomu, utaanza Machi 23 na uchaguzi utafanyika Aprili 30.
Katika ngazi ya tawi, fomu kwa wagombea wa jumuiya zitaanza kutolewa Machi 3 na uchaguzi wake utafanyika Aprili 22, wakati fomu za kuwania uongozi wa chama zitaanza kutolewa Februari 20 na uchaguzi utafanyika Machi 31.
Katika ngazi ya kata, wagombea wa jumuiya wataanza kuchukua fomu Mei 4 na uchaguzi wake ni Juni 30, wakati kwa wagombea wa chama fomu zitaanza kutolewa Mei 13 na uchaguzi utafanyika Julai 4.
Ngazi nyingine Visiwani Zanzibar, fomu kwa ajili ya uchaguzi wa majimbo zitaanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi wake kufanyika Julai 26 kwenye jumuiya na Agosti 2 kwa wagombea wa uongozi wa chama. Kwa upande wa wilaya, ratiba hiyo inaonyesha kwamba fomu za uchaguzi wa viongozi wa wilaya wa jumuiya Tanzania Bara, zitaanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi wake kumalizika Agosti 22, huku fomu kwa ajili ya viongozi wa chama, zikipangwa kuanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi kufanyika Septemba 26.
Taarifa hiyo yenye ratiba ilifafanua kwamba katika ngazi ya mkoa, uchaguzi wa jumuiya utaanza Juni 2 na uchaguzi utafanyika Septemba 26 na fomu za uchaguzi wa viongozi wa chama, zitaanza kutolewa Juni 2 na uchaguzi wake kufanyika Oktoba Mosi mwaka huu.
Ngazi ya taifa, fomu zitaanza kutolewa Juni 2 kwa wagombea wa jumuiya na uchaguzi wake utafanyika Oktoba 5 na fomu kwa ajili ya wagombea wa ngazi ya chama, zitaanza kutolewa Oktoba 25 na uchaguzi utafanyika Novemba 11. Mkutano Mkuu wa taifa unatarajiwa kufanyika Oktoba 9 ili kukamilisha Uchaguzi Mkuu na kuunda Sekretarieti ya Taifa.
|