|
Fidelis Butahe MZIMU wa aliyekuwa Kiongozi wa watu wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi, umeibukia bungeni baada ya Mbunge wa Mbeya mjini Joseph Mbilinyi jana kuitaka serikali ieleze namna uwekezaji wa kiongozi huyo nchini ulivyolinufaisha taifa.
Mbilinyi maarufu kama ‘sugu’ aliluliza swali hilo jana katika kipindi cha maswali na majibu katika kikao cha nne cha Bunge mjini Dodoma, huku Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe akipigilia msumari hoja hiyo kwa kudai kuwa serikali ya Tanzania imekuwa na mtindo wa kuwa na uhusiano na mtu binafsi na si nchi husika. Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji na Uwezeshaji), Dk Mery Nagu alisema kumbukumbu zilizopo Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) zinaonesha kuwa Gaddafi hakuwahi kuwekeza kibiashara nchini.
“Mradi uliopo ni ule wa uwekezaji wa Kampuni ya North Africa Investment Company na hii ni kampuni kutoka nchini Libya sio ya Gaddafi,” alisema Dk Nagu. Alifafanua kwamba kampuni hiyo ndio inayomiliki hoteli ya Bahari Beach iliyopo jijini Dar es Salaam na kwamba kampuni hiyo iliinunua hoteli hiyo mwaka 1998 na kutengeneza ajira 160.
“Gaddafi hakuwekeza kibiashara nchini na wala hakuna anayefaidika na hilo kwa kuwa hana uwekezaji wowote,” alisema Dk Nagu. Pamoja na majibu hayo Mbilinyi aliuliza swali la nyongeza kwamba serikali bado inatakiwa kulifafanua suala hilo kwa kuwa uwekezaji huo ulifanyika wakati Gaddafi akiwa madarakani na kuongeza kuwa serikali ya Tanzania ilisema wazi kuwa haiitambui serikali ya sasa ya Libya.
“Tanzania ilikuwa na urafiki na Gaddafi kama ni hivyo ilizishawishi vipi nchi nyingine baada ya Libya kuvamiwa na majeshi ya NATO?” alihoji Mbilinyi. Akijibu kwa msisitizo, Dk Nagu alisisitiza kuwa Tanzania ilikuwa na uhusiano na Libya lakini uhusiano huo haukuwa baina ya mtu na mtu, bali ni nchi na nchi.
“Bado nasisitiza kwamba Gaddafi hakuwekeza nchini na kampuni hiyo niliyoitaja ipo na inafuata taratibu zote za uwekezaji, nisingependa kuihusisha serikali na mtu binafsi,” alisema Dk Nagu. Baada ya majibu hayo, mjadala huo ulizidi kuwa mzito baada ya Zitto Kabwe kuitaka serikali ieleze kama ilisalimisha mali zote za kiongozi huyo huku akisisitiza serikali imekuwa na utaratibu wa kuwa na uhusiano na mtu binafsi na si wa serikali ya nchi husika, ” tuelezwe kiundani maana serikali imekuwa na mtindo wa kuwa na uhusiano wa ki- Optimistic diplomatic relation”.
Dk Nagu alipinga kauli hiyo kwamba serikali imekuwa na uhusiano na watu binafsi na si serikali za nchi husika, “Kampuni za Libya zimewekeza nchini kibiashara na serikali ya Tanzania ina uhusiano na nchi husika na sio mtu binafsi”. Katika hatua nyingine Waziri wa Ujenzi, Dk John Magufuli alitoa ufafanuzi wa ujenzi wa barabara za mkoa wa Tabora kwa kiwango cha lami wakati akijibu swali la mbunge wa Tabora mjini, Ismail Aden Rage ambaye alitaka kujua kama barabara za mkoa huo zitajengwa kwa kiwango hicho.
Akitoa ufafanuzi huo Magufuli alizitaja barabara hizo kuwa ni ile ya Nzega-Tabora, Tabora-Manyoni na Tabora-Urambo na kwamba zina urefu kwa kilimota 459 na zitakamilika katika kipindi kilichopangwa. Alisema ujenzi huo umechelewa kuanza kutokana na kuchelewa kwa makandarasi pamoja na fedha za kuwalipa.
Alisema serikali bado inaendelea kutafuta fedha za kuwalipa makandarasi hao na kwamba ambazo wameshalipwa ni za awali. “Wananchi wa Tabora wanatakiwa kuwa na imani na serikali ya CCM na barabara hizo zitakwisha katika kipindi cha mwaka 2013 na 2014. Nawahakikishia kwamba makandarasi wasiofaa wataendelea kutimuliwa na serikali kwa kuwa mpaka sasa wameshafukuzwa 2900” alisema Magufuli.
|