MwanzoContactsEmail
Home Habari Mahakamani IGP, Mwanasheria Mkuu waitwa mahakamani
BOOKMARK THIS PAGE
IGP, Mwanasheria Mkuu waitwa mahakamani  Send to a friend
Tuesday, 24 January 2012 20:54

James Magai
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imewataka mahakamani hapo leo, Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ili kutoa maelezo ya kwa nini walimkamata na kumshikilia Kiongozi wa Chama cha Movement for Solidarity and Development (MSD) cha Burundi, Alexis Sinduhije (46).

Amri hiyo ya Mahakama ilitolewa jana na Jaji Lawrence Kaduri baada ya kukubaliana na ombi lililowasilishwa mahakamani hapo na Wakili wa Sinduhije, Hubert Nyange.

Katika maombi hayo namba 7 ya mwaka 2012 yaliyowasilishwa chini ya hati ya kiapo cha dharura, Nyange anadai kuwa kitendo cha Sinduhije kukamatwa na kushikiliwa ni kinyume cha utawala wa sheria na ukiukwaji wa haki za binadamu.
Sinduhije alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) kwa hati ya Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) akitokea Kampala, Uganda kuja nchini na Januari 13 alifikishwa mahakamani Kisutu, lakini hakusomewa mashtaka.

Mtuhumiwa huyo ambaye pia ni mwanzilishi wa Redio Publique Africaine (RPA) ya Burundi, alikamatwa na polisi na kushikiliwa kwa wiki mbili mfulululizo katika Kituo cha Polisi Kati Dar es Salaam, huku kukiwa hakuna maelezo yoyote kutoka serikalini na jeshi hilo kuhusu sababu za kukamatwa kwake.

Wakati akikamatwa na Interpol, Sinduhije alituhumiwa na Serikali ya Burundi kuhusika na mauaji ya Mwakilishi wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa (WHO), Dk Kassi Manlan raia wa Ivory Coast na aliyekuwa mtumishi wake na pia mauaji ya halaiki ya Katumba.

Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo aliyotoa polisi, Sinduhije ambaye pia ni mwandishi wa habari za uchunguzi alidai kuwa ndiye aliyefanya uchunguzi wa mauaji ya Dk Manlan, ambao uliwezesha watuhumiwa kukamatwa na kushtakiwa na kisha kupatikana na hatia.

Kuhusu mauaji ya mtumishi wake, alidai aliuawa na wakala wa Serikali ya Burundi wakimfananisha naye kwa kuwa walikuwa wakimtafuta kumuua yeye.

Mtikila aibuka
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama cha Democratic (DP), Mchungaji Christopher Mtikila amemwandikia barua Rais Jakaya Kikwete akishauri kiongozi huyo aachiwe bila masharti.

Katika barua hiyo, Mtikila amedai kuwa Sinduhije hakuhusika na tuhuma za mauaji zinazomkabili nchini mwake na badala yake ndiye aliyefanya uchunguzi wa kifo cha Dk Manlan na kukibainisha.

“Inajulikana wazi kwamba mtumishi wa Sinduhije aliuawa na wakala wa Serikali kwa makosa wakidhani kuwa wamemuua Alexis Sinduhije mwenyewe,” alisema Mtikila kwenye barua hiyo.

Aliongeza kwamba, Sinduhije hakuhusika na mauaji ya Katumba kwa kuwa wakati mauaji hayo yakitokea Novemba mwaka jana, kiongozi huyo wa MSD hakuwepo Burundi baada ya kukimbia kutokana na uhasama wa kisiasa baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Akizungumzia barua hiyo, Mtikila alisema alipoipeleka Ikulu aliambiwa kuwa Rais Kikwete hakuwepo na kushauriwa kuwasiliana na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Sinduhije alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Januari 13 mwaka huu, lakini hakusomewa mashtaka na badala yake alirudishwa mahabusu katika Kituo Kikuu cha Polisi  ambako alikuwa akishikiliwa bila kupelekwa mahakamani.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #3 2012-01-25 14:01
IGP fidia atalipa yeye
au kodi zetu?
Quote
 
 
0 #2 2012-01-25 13:31
IGP Mwema alipata taarifa za kiintelijensia.
Quote
 
 
0 #1 2012-01-25 10:57
Tanzania Zengwe jingine hilo litatufanya tulipe fidia kwa US Dollars.

Watendaji wetu tafadhalini nendeni shule hamjachelewa! Kisheria ni kosa kumshikiria mtu kizuizini bila kosa.
Serikali wapeni nafasi hizi za Ukuu wa polisi watu wenye uwezo wa kujua sheria.

Mtu mwenye wafuasi wengi katika congregation yake na hata chama cha siasa kama Mtikila inashangaza anavyojiingiza katka hili- Mtikila nafasi yako ni ipi katika hili?

Watanzania tujifunze kuwapa uongozi watu wanaofanya maamuzi kwa kujua walitendalo.
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner