|
Kigogo wa BoT kizimbani tena |
Send to a friend |
|
Monday, 30 January 2012 20:40 |
|
Nora Damian NAIBU Mkurugenzi wa Mifumo na Huduma katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Simon Jengo, amepandishwa kizimbani akikabiliwa na mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi katika ununuzi wa mashine 26 za kuharibu noti.
Kigogo huyo alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Jengo anyeakabiliwa pia na kesi nyingine katika Mahakama ya Wilaya Ilala, anatuhumiwa kughushi nyaraka kwa kampuni inayotengeneza noti za benki hiyo kwa lengo la kumdanganya mwajiri wake na kumsababishia hasara ya zaidi ya Sh 104 bilioni.Mwendesha Mashtaka wa Takukuru Ben Lincon, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Rita Tarimo kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo kati ya Januari mwaa 2005 na Desemba mwaka 2008 katika makao makuu ya BoT.
Alidai kuwa mshtakiwa alimshauri vibaya Gavana wa BoT katika ununuzi wa mashine 26 za kuharibu noti pasipo kujali mahitaji halisi ya benki. Hata hivyo mshtakiwa alikana mashtaka na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi bado haujakamilika na kwamba hawana pingamizi na dhamana.
Hakimu Tarimo alitoa masharti ya dhamana ambapo mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika watakaosaini dhamana ya maneno ya Sh 10 milioni kila mmoja.
Jengo alitimiza masharti hayo na kuachiwa kwa dhamana hadi kesi Februari 29 mwaka huu, kesi hiyo itakapotajwa tena. Katika kesi iliyoko Mahakama ya Ilala, Jengo anashtakiwa na maofisa wengine watatu wa BoT akidaiwa kughushi nyaraka kwa kampuni inayotengeneza noti za benki hiyo kwa lengo la kumdanganya mwajiri wao. Washtakiwa wengine ni Kisima Mkango, Bosco Kimela na Ally Farjallah Bakari ambao kwa pamoja wanadaiwa kutenda makosa hayo jijini Dar es Salaam.
Wanadaiwa kuwasilisha nyaraka kwa kampuni hiyo ili kuchapisha kiasi kikubwa cha noti tofauti na kilichoidhinishwa na mwajiri wao.
Katika mashtaka mengine wanadaiwa kuingia mkataba wa kuchapa noti kwa bei ya juu kinyume na makubaliano halali hivyo kuisababishia Serikali hasara ya Sh 104,158,536,146.
Wanadaiwa pia kuupeleka mkataba huo kwa mamlaka zinazotengeneza noti ukionyesha bei ya uongo
|
Comments
naomba mamlaka husika wafuate taratibu zinazotakiwa na mwisho wa siku,watu kama hawa watangazwe kwa umma ili umma ujifunze.
ahsante sana mwananchi gazeti kwa taarifa hii nzuri,endeleeni kutujuza zaidi,upo uozo mwingi sana kwenye taasisi za serikali,hata kuhusu yule mkurugenzi wa TBS mbona kimya hamtuambii tena?wananchi tunahitaji kujua kama kweli bunge wanachosema ni sahihi au yeye ndo yupo sahihi.TBS ni nyeti sana kama uozo kama huo unatendeka pale,habari gari juu ya bidhaa feki ambazo hazina hata make wala made in where zimejaa kariakoo wala hakuna hata mtu anayefuatilia.pengine ndo mradi wao?
tafadahri tupeni habari wadau.