MwanzoContactsEmail
Home Habari Mahakamani Upelelezi kesi ya dawa za kulevya ya Mama Leila haujakamilika
BOOKMARK THIS PAGE
Upelelezi kesi ya dawa za kulevya ya Mama Leila haujakamilika  Send to a friend
Thursday, 02 February 2012 07:50

Tausi Ally
UPELELEZI wa kesi ya kuingiza nchini kilo tano za dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye thamani ya Sh225 milioni inayomkabili Mwanaidi Mfundo anayejulikana pia kwa jina la Naima Mohammed Nyakiniwa au Mama Leila aliyetajwa pia na Rais Barack Obama wa Marekani kama mtu hatari kwa biashara hiyo bado haujakamilika.
Hayo yalielezwa jana mbele ya hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Augustina Mmbando na Wakili wa Serikali, Kenneth Semkwao wakati kesi hiyo ilipotajwa.  

Wakili Semkwao alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo kwa sasa bado haujakamilika lakini unakaribia kukamilika.
Baada ya kutoa maelezo hayo, Wakili anayewatetea washtakiwa hao, Evod Herman alidai kuwa mara nyingi upande wa mashtaka umekuwa ukidai kuwa upelelezi unakaribia kukamilika  na kwamba hii ni mara ya sita kudai hivyo.

Wakili Herman alihoji muda wa kukamilika kwa upelelezi huo kwa madai kuwa wateja wake wamekuwa rumande kwa takribani mwaka sasa.

Wakili wa Serikali akijibu hoja hizo, alidai kuwa hoja hizo ni za msingi  lakini hawezi kuzungumzia  kwa undani  upelelezi umefikia wapi  kwa sababu alikuwa na nakala ya jalada na siyo jalada halisi.

Hivyo aliiomba mahakama aipangie tarehe nyingine ili aweze kufuatilia kinachoendelea na kuongeza kuwa wakili Herman anayo njia  nyingine  ya kuandika barua kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kama wanaona upelelezi unachelewa.
Baada ya kutoa maelezo hayo, wakili Herman alimjibu wakili mwenza kuwa yeye ndiye mwakilishi wa DPP afikishe ujumbe.

Hakimu Mmbando naye pia aliutaka upande wa mashtaka kufuatilia upelelezi umefikia wapi na kesi hiyo imepangwa kutajwa tena Februari 14, mwaka huu.

Awali Juni 3, mwaka jana watuhumiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza mahakamani wakikabiliwa na shtaka la kuingiza nchini kilo tano za dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani ya Sh225 milioni.  

Wakili wa Serikali, Patrick Malogoi alidai mbele ya Hakimu Mustapha Siyani, kuwa Juni Mosi, mwaka jana maeneo ya Mbezi Beach washtakiwa hao kwa pamoja kinyume na kifungu cha 16 (1) b (i) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, sura ya 95 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2009, waliingiza nchini dawa hizo za kulevya.

 Baada ya kuwasomea shtaka hilo, Hakimu Siyani aliwataka washtakiwa hao kutojibu chochote kwa sababu Mahakama ya Kisutu haina mamlaka ya kusikiliza shtaka linalowakabili hadi Mahakama Kuu ya Tanzania.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner