
| Wabunge wazoa Sh90mil kila mmoja | Send to a friend |
| Tuesday, 15 February 2011 07:35 |
|
JUMLA ya Sh3.24 bilioni zimelipwa kwa wabunge ili kuwawezesha kununua magari binafsi kwa ajili ya shughuli za kibunge, imeelezwa. Kwa mujibu wa habari hizo kila mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amelipwa Sh90 kwa ajili ya kujinunulia gari. Aidha, wabunge hao wapatao 360 wamekatiwa bima ya afya inayotarajiwa kuanza kutumika kabla ya mwezi Juni mwaka huu. Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika uzinduzi wa Tawi la Chadema, Mipango Kata ya Miyuji mkoani Dodoma wabunge wa Chadema, walisema kuwa wanashangazwa na hatua ya Rais Kikwete kuweka pikipiki za matairi matatu (Bajaji) kama moja ya vipaumbele vyake ili zitumike kubeba wajawazito wakati wabunge wanalipwa mamilioni. Katika hotuba yake ya kulizindua bunge Kikwete alieleza mpango wa serikali yake kununua pikipiki hizo 400 zitakazosambazwa maeneo mbalimbali hasa vijijini kwa ajili ya kuwabebea wajawazito kama njia ya kupunguza matatizo ya usafiri kwenye maeneo hayo. "Ndugu zangu hali ni mbaya, siku moja tutafanya maandamano bungeni, sio kutoka nje ya ukumbi. Inashangaza, tumepewa Sh90 milioni za magari kwa wabunge wote, huku bungeni tunajadili bajaji kuwa 'ambulance'(gari ya kubebea wagonjwa),'" alisema mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema. Alisema mbali na hilo katika hali inayoonyesha kuwa hospitali za serikali ni mbaya, katika semina iliyofanyika Dar es Salaam hivi karibuni, wabunge waliomba kuwekewa bima za afya, kutibiwa nje ya nchi na katika hospitali binafsi hapa nchini. "..Wabunge tumeomba 'insurance' (Bima) kila mmoja amepewa na kabla ya Juni naamini zitaanza kutumika, tumeomba kutibiwa 'private hospital' (hospitali binafsi). Hii inaonyesha hospitali za serikali zilivyo mbaya na hao wenye uwezo wanazikimbia," alisema Lema. Aliongeza kuwa: Ndoto ya kuiondoa CCM ni 'serious' (thabiti), lakini mkifanya noma ya kupata haki, hiyo imebarikiwa. Kama (CCM) wanafikiri wanaweza kuendesha nchi watakavyo, sasa hawawezi, ninyi vijana msipojitoa kwa sasa nchi itakufa." Alikwenda mbali zaidi akisema anaomba wake za viongozi wapate ujauzito na kupakiwa katika bajaji hizo wakati wa uchungu kwenda kujifungua ili waone adha ya usafiri huo itakavyokuwa. Akiongea katika mkutano huo naye mbunge Tundu Lissu aliwataka wananchi kutoogopa mabadiliko na kwamba historia haiheshimu watu wanaoogopa. ""Historia haiheshimu wanaoogopa, tusije kusahau bei ya mabadiliko, bei yake ni kupigwa, kufungwa hata bei kubwa zaidi ya kifo," alisema Lissu. Naye John Mnyika alisema Chama chake kitaandaa kongamano maalumu la vijana wa vyuo vikuu ili wapate muda wa kuzungumza nao vizuri na kwamba maandamano ya kuishia viwanjani yametosha na sasa watakuwa wakifika kwa wahusika. "..Maandamano ya kuishia viwanjani imetosha, sasa tutaenda maeneo ya wahusika, vyuo lazima mjenge mtandao imara, lazima mpambane na umasikini," alisema Mnyika. |
















Comments
300 X Tshs.90,000,000/= ni TshsBilioni 27
Wito wangu ni kwa vyama vya upinzani kupeleka magari hayo yakatumike kwenye majimbo yoa, nadhani serikali itaona aibu.
Kwakweli kwa style hii, lazima 2015 nitangaze nia.
jamani hivi pesa hizo ,tungeongea na serikali ya japan au germany au kokote mtu afikiriapo, tukawaomba kununua magari ya wabunge kweli ingeshindikana, na pesa zingetumika nyingi namna hiyo?hivi jamani tusioneane aibu, ni nchi gani inayotoa magari ya bei kubwa namna hiyo? nijuavyo mm nchi kadhaa,ukikutan a na wawakilishi wao bungeni unaweza kuona huruma,kama ni daladala wote daladala.sio kusema wasiwe na magari yao, hapana, ila yasiwe ya bei kubwa sana jamani,ina maana baada ya miaka 5 tena wanapewa nyingine!!? kudadeki..eti nchi masikini?
kuna watu hawajui hata umeme ni nini ?
watu hawajui hata maji ya bombani ni nini?
watu hawajui hata hospitali zipo wapi zaidi ya dispensari tu.embu fikirieni upya nyang'au nyie...!
Mungu atainua majemedari watakaosimama nawe pamoja na wengine kama Dr Slaa, Mbowe, Mnyika, Mdee na wengine wanaosononeka juu ya umasikini unaoendelezwa na watawala walioko madarakani. Pamoja tutasimama na kushinda. Ngoma ya utawala sasa inalia sana maana kupasuka kwake kumekaribia. Mungu ibariki Tanzania.