MwanzoContactsEmail
Home Habari Uchumi na Biashara Madereva wa malori waanza mgomo
BOOKMARK THIS PAGE
Madereva wa malori waanza mgomo  Send to a friend
Tuesday, 17 January 2012 21:18

Waandishi Wetu
CHAMA cha Madereva wa Malori Tanzania (Chamamata) kimepuuza wito wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) wa kuwataka kuacha kugoma badala yake jana walianza rasmi mgomo huo.

Madereva hao wa malori walianza mgomo huo nchi nzima wakilalamikia waajiri wao kwamba wamekuwa hawazingatii maslahi yao.

Mgomo huo ulianzia Tunduma, yalipo makao makuu ya Chamamata na kuenea nchi nzima na taarifa zilisema madereva wengi waliokuwa safarini waliegesha malori wakisubiri chama kitoe tamko.

Sumatra, jana ilikuwa inafanya kila njia ya kutaka kuuzima mgomo huo kwa kuwasiliana na Chamamata lakini hadi jioni, ilikuwa haijafanikiwa.

“Mgomo huu ni wa muda tu. Tumekuwa tukifanya juhudi za kuwashawishi wasiendelee na mgomo huo. Baada ya muda utaisha na walio safarini wataendelea kama kawaida,” alisema Meneja wa Leseni wa Sumatra, Leo Kumbuka.

Akizungumzia mpango wa kutatua mgogoro huo, Kumbuka alisema Sumatra inafanya tathmini ya tatizo la mgogoro huo kwa kuzungumza moja kwa moja na madereva.

Alisema wameweka vituo vitatu, Kibaha, Dodoma na Tunduma na kwamba mkakati huo ulimalizika jana na baada ya kukusanya maelezo hayo, Sumatra itachukua hatua.

Mwenyekiti wa Chamamata, Rocket Matogolo ambaye anadaiwa alikuwa mafichoni Tunduma, hakupatikana kwani alikuwa amezima simu yake ya mkononi na watu walio karibu naye walisema alifanya hivyo kuepuka kurubuniwa ili asitishe mgomo.

“Huu mgomo yaelekea umesababisha matatizo mengi na madereva hawapo tayari kuendelea na safari hadi hapo watakapopata maelekezo kutoka kwa mwenyekiti,” alisema mmoja wa watu hao walio karibu na Matogolo na kuongeza:

“Lakini hapa mwenyekiti amepata usumbufu mwingi mpaka kuna watu wamempigia na kumwambia wapo tayari kumpa Sh150 milioni ili asitishe mgomo huo, lakini amekataa. Hapa yupo kwenye mkutano na ameapa, hatawasha simu na hataki kurubuniwa. Anajadiliana na watu na siyo rahisi watu kupajua kwa sababu eneo hili amekwenda kwa siri.”

Alifafanua kwamba, madereva wanaogoma wapo wasio na mikataba na wapo walio nayo, lakini wamebaini kisheria haina nguvu na imetengenezwa kwa maslahi ya wamiliki wa malori.

Mmoja wa madereva wenye mkataba ambaye hakutaka kutajwa jina alisema wengi wanalipwa kati ya Sh150,000 hadi Sh200,000 na posho ndogo zisizozingatia kama dereva anafanya safari ndani ya nchi au nje.

Alisema wanachotaka ni kima cha chini cha mshahara kisipungue Sh500,000 na viwango vipya vya posho vizingatie umbali na ugumu wa mazingira ya kazi wakisema kama ni nje ya nchi, wapewe kwa fedha za kigeni za nchi wanayokwenda au ziwe kwenye Dola za Marekani.

Jumamosi iliyopita, Matogolo aliliambia gazeti hili kwamba Sumatra imeudanganya umma kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu  mikataba ya madereva.

“Sumatra wanatakiwa kuwa wa kweli kwa hili kwani inaweza kusababisha usumbufu kutokana na kulinda maslahi ya watu fulani (matajiri). Kama kawaida yetu migomo yetu hufanyika Tunduma na Sumatra wanasema wametoa mikataba tunawataka waje kuwaonyesha madereva na siyo kukaa na kuupotosha umma,” alisema Matogoro.

Wiki iliyopita, Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka hiyo, Ahmad Kilima alitoa wito kwa madereva hao kusitisha mpango wao wa kugoma na badala yake kuwasilisha malalamiko yao kwao.

Kilima alisema mgomo huo, unaweza ukazua matatizo makubwa kama vile madereva kutelekeza malori barabarani na kusababisha hasara kwa wamiliki jambo ambalo alilielezea kuwa ni kosa la jinai.

Alisema tangu mwaka 2009, mamlaka hiyo imekuwa ikitumia kigezo cha mkataba wa ajira kama moja ya sharti la kupewa leseni ya usafirishaji lakini akashangaa kusikia madereva wengi hawana.

“Labda, kuna tatizo jingine kwa sababu kama mikataba iko mingi tu na hakuna dereva yoyote aliyewahi kujitokeza na kusema kuwa hana mkataba wanalalamika mitaani tu,” alisema Kilima.

Habari hii imeandaliwa na Leon Bahati Dar na Stephen Simbeye, Tunduma.

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner