|
Madereva wa malori waligoma wadokezwa siri |
Send to a friend |
|
Wednesday, 18 January 2012 20:47 |
|
Stephano Simbeye, Mbozi MAMLAKA ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi kavu na Majini (Sumatra) imewashauri madereva wa malori ambao wapo kwenye mgomo kujiunga kwenye Chama cha Wafanyakazi ili chama hicho kiweze kushughulikia madai yao huku wao wakiendelea na kazi zao.
Ushauri huo ulitolea jana na Mkurugenzi wa Kanuni na Usafirishaji wa Barabarani, Amon Kisaka alipozungumza na viongozi wa umoja wa madereva katika Kituo cha Polisi mjini Tunduma mkoani Mbeya.
Alisema kwa kufanya hivyo kutawarahisishia mawasiliano baina yao na Serikali kwa kuwa chama hicho kinatambulika na Serikali badala ya kuendelea na mgomo.
Alisema Sumatra inatambua madai yao kuwa ni ya msingi na kuwa madereva wanapaswa kujaza fomu zilizotolewa kwao ili iweze kwenda kulinganisha na mikataba iliyoonyeshwa na wamiliki wa malori hao walioionyesha kwa mamlaka hiyo, lakini katika kipindi ambacho suala hilo linashughulikiwa aliwataka waendelee na safari zao kama kawaida. “Iwapo mtajaza fomu hizi Sumatra itajua namna ya kuwabana wamiliki wa malori ili kuweza kubaini ukweli wa madai kuwa mikataba iliyopo Sumatra ni feki au la ambayo itasaidia kwa kuwa sisi hatuna taarifa zenu” alisema Kisaka.
Mkurugenzi huyo alisema Sumatra inashindwa kuwasaidia kama wanavyotaka wao kwa vile hawatambuliki kisheria, hivyo kuwashauri wajiunge katika chama cha wafanyakazi kilichopo ama waunde chama chao ili wavitumie kudai haki zao. Hata hivyo alisema itahakikisha wanapata mikataba ya ajira na kuwa taarifa itatolewa kwenye vyombo vya habari mara tu atakapofika Dar es salaam.
Rashidi Salehe, mmoja wa madereva hao akizungumza kwa niaba ya wenzake alisema madereva hawana ugomvi na Serikali wala waajiri wao, bali wanachotaka ni kuboreshewa maslahi yao na mazingira mazuri katika kazi ambapo wamekuwa wakifanya kazi pasipo kupata stahili sahihi za safari, ikiwa ni pamoja na uhakika wa ajira kwani utaratibu uliopo hivi sasa mfanyakazi anaweza kufukuzwa wakati wowote na mahali popote na akakosa mahali pa kudai haki zake.
“Hawa matajiri wanatumia nguvu ya fedha kuwadhoofisha madereva kwa kuwasambaratisha lakini iwapo Sumatra itasimama imara itatusaidia kuweza kutengeneza mazingira ya kupatikana haki zetu,” alisema Salehe.
Aidha mmoja wa aliyekuwa kiongozi katika mgomo uliopita Isaack Emmanuel alisema tatizo la madereva ni kutokuwa watulivu kwani mazungumzo yaliyokwishaanza baina ya Serikali na waajiri yanakwenda vizuri, lakini kutokana na uelewa mdogo wameamua kutafuta uongozi mwingine ambao haujui hatua iliyokwishafikiwa na hivyo kulifanya jambo hilo kuwa jipya.
“Madereva wanajichanganya wenyewe wakiwa huku wanajifanya wana misimamo, lakini wanapofika kwa waajiri wao wanaogopa kuzungumza nao kutokana na hofu ya kufukuzwa kazi jambo ambalo linasababisha usumbufu kwa Watanzania wengine” alisema Emmanuel. Leo ni siku ya tatu tangu mgomo huo kuanza ambapo jitihada za Serikali zinaendelea kujaribu kuwashawishi madereva hao wasitishe mgomo wao ambao umesababisha msongamano usiokuwa wa lazima katika Mji wa Tunduma.
|
Comments
Serikali itafute suluhisho la kudumu kuhusu migomo ya mara kwa mara. Kutumia nguvu na maneno ya vitisho siyo dawa, hawa ni watu wazima na wana uelewa. Hivyo kuwadanganya haitasaidia kitu. Mwaka jana kulikuwa na mgomo kama huu na Serikali ilitoa ahadi ya kufuatilia suala lao kwa kipindi cha mwezi mmoja lakini bado hadi kipindi hiki hakuna kilichofanyika, na ndio maana wameamua kugoma tena ili kufikisha ujumbe wao kuwa hawakutendewa haki. Na sasa tunaona tena Serikali inaahidi kushughulikia kipindi cha mwezi mmoja na ikiwa mwaka jana walishindwa toka mwezi Oktoba 2011 hadi hii Januari 2012!!!!!
Sheria zimewekwa na Serikali inakuwaje wanashindwa kufuata sheria zilizopitishwa na Bunge katika [NENO BAYA]liza suala hili?
Kwani kwa mtazamo wangu hili suala limekaa Kisheria mno.
Waajiri pia wasiwe na tabia ya kutishia wafanyakazi eti mtu akionekana anadai haki au ni msemaji sana wanaamua kumfukuza kazi.
Katika suala hili la mgomo kama huu, hasara zipo pande zote:-
(1) Serikali inapata hasara kubwa kwani pesa ya ushuru inakosekana ambayo inakusanywa kila siku.
(2) Waajiri wanapata hasara kwani magari hayaendi katika mzunguko kama ilivyo kawaida .
(3) Bandari inapata hasara kwani mizigo haitoki na kusababisha msongamano.
(4) Nchi jirani (ambao ndio wateja wetu) wanapata hasara kwani hawapati mizigo yao kwa wakati. mfano: bidhaa ya mafuta ambayo nchi kama Zambia na Congo zinategemea Bandari ya DSM, nchi hizi zinakumbwa na uhaba wa bidhaa hii muhimu kwa uchumi wa nchi zao.
(5)Madreva nao wana pata hasara kwani siku wanazokaa pale mpakani wanaishi kwa shida kutokana na kuishiwa pesa za matumizi.
Hivyo ni wajibu wa kila mmoja anayehusika katika kusababisha mgomo huu aangalie njia itakayoleta suluhu na siyo ubabe HAUTASAIDIA.
Jamani tuwe na ubinadamu sote ni ndugu ingawa hatukuzaliwa katika familiya moja!!!!
JULIAN C. M.
INANIUMA SANA!!!!