53 mbaroni wakidaiwa kufanya matukio ya ugaidi Kilindi

Muktasari:

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema juzi kuwa idadi hiyo inajumuisha watuhumiwa waliokamatwa mwaka juzi Kilindi na wengine waliohusishwa na matukio ya uhalifu katika mapango ya Amboni jijini Tanga huku baadhi yao wakinaswa nchini Kenya.

Tanga. Watuhumiwa 53 wa matukio yenye viashiria vya ugaidi yaliyotokea wilaya za Kilindi na Amboni mkoani Tanga, wapo katika mahabusu za magereza wakisubiri michakato ya kusikilizwa kesi zao pamoja na hukumu.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Benedict Wakulyamba amesema juzi kuwa idadi hiyo inajumuisha watuhumiwa waliokamatwa mwaka juzi Kilindi na wengine waliohusishwa na matukio ya uhalifu katika mapango ya Amboni jijini Tanga huku baadhi yao wakinaswa nchini Kenya.

Wakulyamba amesema hayo  wakati akitoa taarifa ya hali ya ulinzi na usalama mkoani hapa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba alipowasili kwa ziara ya kikazi.

Amesema Aprili 20, wakazi wa Mkoa wa Tanga na Tanzania kwa ujumla walikuwa katika wakati mgumu, kufuatia kundi la wahalifu hao kuvamia duka la Central Bakery na kuwaua kwa kuwapiga risasi watu wanne.