66,000 wakosa mikopo

Wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliochaguliwa kujiunga na Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es salaam wakisubiri kufanyiwa udahiri chuoni hapo,  Mwenge jijini Dar es salaam juzi. Picha na Ericky Boniphace

Muktasari:

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), wengi hawatapata.

Dar es Salaam. Ahadi iliyotolewa na Rais John Magufuli wakati wa kampeni mwaka jana kwamba katika Serikali yake hakuna mwanafunzi atakayekosa mkopo wa masomo ya elimu ya juu imekuwa ngumu kutekelezeka.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kwamba kati ya wanafunzi 88,000 walioomba mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), wengi hawatapata.

Uwezo wa bodi hiyo ni kutoa mikopo kwa wanafunzi 21,500 pekee sawa na asilimia 24 na waliopatiwa hadi sasa ni wanafunzi 11,000 sawa na asilimia 12.

Takwimu hizi zinaonyesha kwamba zaidi ya robo tatu ya wanafunzi wanaohitaji mikopo watakosa kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.

Akizungumza wakati wa kampeni za urais mwishoni mwa mwaka jana mkoani Tabora, Dk Magufuli ambaye alikuwa mgombea kwa tiketi ya CCM, alisema katika Serikali atakayounda kiongozi ambaye atamchelewesha mwanafunzi kumpa mkopo ajue kazi hana.

Katika kuhakikisha anaweka mambo sawa kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu, Serikali ya Rais Magufuli kupitia kwa Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, alimfutia mkataba wa kazi Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, George Nyatenga na nafasi yake ikachukuliwa na Abdul Razaq Badru.

Jana, mkurugenzi huyo alipoulizwa Bodi yake imetoa mikopo kwa wanafunzi wangapi wa elimu ya juu alisema, “Tayari awamu ya kwanza inayohusisha jumla ya wanafunzi 11,000 wamepatiwa mikopo, lengo letu mwaka huu ni kutoa mikopo kwa wanafunzi 21,500.”

Pia, alipoulizwa kuhusu suala la wanafunzi kuchelewa kupatiwa mikopo, mkurugenzi huyo alisema kuwapo kwa ucheleweshaji huo ni kutokana na mazingira fulani fulani ambayo hata hivyo, hakuwa tayari kuyataja bayana.

Kwa mujibu wa Badru, hali ilikuwa mbaya zaidi kipindi cha nyuma ambapo ilikuwa ikichukua hadi zaidi ya miezi miwili au mitatu lakini sasa bodi hiyo imepunguza muda huo na sasa imetumia siku nne pekee.

“Ni kweli mwanzoni kulikuwa kuna ucheleweshwaji lakini kasi iliyotumika mwaka huu huwezi kulinganisha na miaka mingine kwani tumeanza mchakato wa kupata majina siku nne zilizopita na jana tu wanafunzi wameshaanza kulipwa fedha zao.

“Tunajua vipo baadhi ya vyuo ambavyo vimefunguliwa wiki mbili zilizopita lakini bodi imeanza jana kutoa hundi kwa wanafunzi wote wa awamu ya kwanza hivyo wasiwe na wasiwasi kila mmoja anayestahili atapata mkopo,”alisisitiza Mkurugenzi.

Badru alisema kwa sasa watumishi wa bodi hiyo wanafanya kazi usiku na mchana ili kuhakikisha kila mwanafunzi anayestahili mkopo anapata kwa wakati.

“Hapa sisi hatulali, kama kuna wanaozimia wazimie ilimradi hospitali zipo tutawapeleka hospitali na kama kuna anayenyonyesha tutamuomba aje na mtoto wake anyonyeshe hapahapa mradi tuwasaidie watoto wa Watanzania wenzetu wapate fedha na kuendelea na masomo yao,” alifafanua.

Alipoulizwa ni wanafunzi wangapi waliotimiza msharti ya kupatiwa mikopo, mkurugenzi huyo alisema wengi walikuwa na sifa lakini walichoangalia ni kutoa fursa kulingana na kipaumbele na rasilimali za Serikali ili kuwekeza kimkakati yaani kuwa na ulinganifu katika nyanja zote.

Alisema kwa kawaida Taifa linahitaji watu wa kada zote na ni ukweli usiopingika kuwa ni lazima kufuata mfumo wa pembetatu unaoelekea juu ikiwa na maana kuwa watu wa kada za juu wachache, wasaidizi na wanaongezeka na wale wa kada ya chini wakiwa wengi zaidi.

“Mfano katika taasisi mbalimbali kama hospitali unakuta madaktari wachache sana, lakini wanaofuata ambao ni maofisa wa kliniki wanaongezeka na unapofika kwa manesi utakuta wengi zaidi,”alieleza.

Alisema jambo jingine walilozingatia katika kutoa mikopo hiyo ni kwa baadhi ya taaluma ambazo zina uhaba zaidi ya watu kama wahandisi, madaktari na wataalamu wa mafuta na gesi hivyo kuona umuhimu wa kuwapa kipaumbele katika mikopo hiyo.

Badru alisema taasisi yake ina jukumu la kutoa mikopo na si lazima kuwasiliana kwanza na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ambao majukumu yao ni kudahili wanafunzi wote wanaojilipia na wanaolipiwa kwa njia ya mkopo na bodi hiyo.

“Kwa kawaida sisi tunatoa matangazo na kutoa vigezo kwa wanaohitaji kupatiwa mikopo waombe, hivyo wanaleta majina bodi na wale wenye vigezo tunawapatia. Tunaanza kutangaza kabla hata TCU haijaanza kufanya udahili na mara tu wanapokamilisha wanatuletea majina ambayo ndiyo tunayafanyia kazi na kuwapa mikopo wote wanaostahili,” alisisitiza Badru.

Tayari TCU imetangaza kukamilika awamu ya kwanza ya udahili kwa waliomaliza kidato cha sita na wenye vyeti vya nje ya nchi.

Kwa mujibu wa tovuti ya TCU, jumla ya waombaji waliosajiliwa mwaka huu ni 55,347 wenye sifa waliopata nafasi ya chuo ni 30,731 na waombaji ambao hawakupata nafasi ni 24,616.

Tume hiyo imeeleza kuwa waombaji wengi wamekosa nafasi katika vyuo kwa sababu ya ushindani uliokuwapo kutokana na uhaba wa nafasi katika kozi hizo. TCU ililazimika kuongeza muda wa udahili kuanzia Septemba 12 hadi 23, 2016 kwa waombaji wenye sifa ili wapate kuchagua kozi zenye nafasi.

*Nyongeza na Muyonga Jumanne