ACT Wazalendo yaandika barua kwa Museveni

Rais wa Uganda Yoweri Museveni

Muktasari:

  • Ni kuhusu kushikiliwa kwa ‘Bobi Wine’

Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kimemwandikia barua, Rais wa Uganda Yoweri Museveni, kikitaka misingi ya sheria na haki za binadamu kufuatwa.

ACT-Wazalendo imeandika barua leo Agosti 20, 2018 baada ya kushambuliwa mbunge Robert Kyagulanyi ‘Bobi Wine’ anayeshikiliwa katika gereza la kijeshi la Makindye, jijini Kampala nchini Uganda.

Bobi na wabunge wengine sita wamefunguliwa mashtaka wakidaiwa kutaka kuipindua Serikali ya Rais Museveni kutokana na vurugu zilizotokea wakati wa kampeni katika uchaguzi mdogo wa Arua, Kaskazini mwa Uganda.

Katika barua hiyo, ACT Wazalendo imesema imepokea kwa mshtuko tukio la kushambuliwa Bobi Wine aliyekuwa akimuunga mkono, mgombea wa Arua, Kassiano Wadri wakati wa kampeni za uchaguzi.

Barua hiyo iliyosainiwa na Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe imetaka Rais Museveni kuwafutia mashtaka wabunge hao na kuhakikisha waathirika wote wa tukio hilo wanapatiwa matibabu.

“Chama cha NRM hakitakiwi kukaa kimya kutokana na vurugu zilizoonyeshwa na Polisi na wanajeshi wa Uganda hivi karibuni dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu, na hasa kwa wawakilishi wa Bunge nchini Uganda,” imesema barua hiyo.