Sunday, November 19, 2017

ACT waahidi kuwalipia ada wanafunzi

 

By Johari Shani, Mwananchi mwananchipapers@mwaanchi.co.tz

Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo Zitto Kabwe, amewataka wananchi wa kata ya  Mhandu jijini Mwanza kumchagua mgombea udiwani kupitia chama hicho Emiry Balahula ili kuleta mabadiliko ndani ya kata hiyo.

Zitto amesema kata hiyo imekuwa na changamoto za miundombinu ya barabara umeme, maji afya na soko.

"Hii wilaya (Nyamagana) ina jumla ya minara 44 ya simu inayolipiwa kodi  hivyo tutatumia fedha hizo kuwalipia ada wanafunzi wa kidato cha tano na  sita," amesema Kabwe

Katibu Mkuu wa Chadema Dk Vicent Mashinji akimnadi  mgombea wa Chadema kata ya Kijima wilayani Misungwi, Gabriel Hiti katika viwanja vya shule ya msingi Mwamaguha, amesema wakimchagua mgombea wa chama hicho watahakikisha wanaibadilisha kata hiyo kwa maendeleo.

Amesema endapo watamchagua  Hiti, kwa kushirikiana na ofisi yake wataanza na uchimbaji wa visima virefu vya maji na kuhakikisha kunakuwepo na uvunaji wa maji ya mvua ili kuitatua changamoto hiyo.

Wakati huohuo Katibu CCM Mkoa wa Mwanza, Raymond Mangwalla, akimnadi mgombea wa chama hicho, kata ya Mhandu wilayani Nyamagana, Sima Costantine amesema  wakimchagua mgombea huyo kero mbalimbali zinazowakabili zitakwisha.

 “Nikichaguliwa mimi nitaanza kuboresha nyumba za walimu, kumalizia jengo la zahanati ya kata na  kuleta vifaa tiba katika zahanati hiyo, “ amesema mgombea wa CCM Kanzaga Ezekieli  kata ya Kijima wilayani Misungwi

-->