ADC yataka Serikali iruhusu mikutano ya kisiasa

Katibu Mkuu wa chama cha ADC,  Doyo Hassan Doyo

Muktasari:

  • ADC wamesema zuio hilo linavinyima vyama vya siasa uhuru na nafasi ya kutangaza sera na mipango yao kwa wananchi.

Dar es Salaam. Chama cha Alliance For Democratic Change (ADC), kimeiomba Serikali kuondoa zuio lililowekwa kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara ya kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Julai 16, Katibu Mkuu wa chama hicho,  Doyo Hassan Doyo amesema zuio hilo linavinyima uhuru vyama vya siasa  kutangaza sera na mipango yao.

"Hali ya kisiasa si nzuri sana, kuna hali ya kutopata uhuru wa kufanya siasa na hasa kwa vyama vya upinzani. Kwa mfano, kuzuiwa kufanya mikutano ya kisiasa na makongamano," amesema.

Doyo pia amewataka wanachama wa CUF ambao wamegawanyika pande mbili, moja ikiongozwa na Mwenyekiti anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba na wa pili ukiongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad, kukaa chini na kumaliza malumbano yao ya kisiasa.

"Chama chetu kinachukizwa na hali inayoendelea ndani ya CUF. Kuendelea kwa mgogoro huo kwa muda mrefu ni kuondoa afya ya upinzani nchini," amesema.