ADL: Mapato yamekua hadi Sh 8 bilioni 2017

Mkurugenzi mtendaji wa kampuni ya usafirishaji mizigo na vifurushi, Frederick Mlay akionyesha tuzo ya ushiriki wa kampuni hiyo kwenye mashindano ya Top 100. Picha na Gadiosa Lamtey.

Muktasari:

  • Kampuni nyingi zilizoshiriki mashindano ya Top 100 kwa miaka saba iliyopita zinafurahia matunda ya jukwaa hilo jinsi lilivyoziongezea uaminifu kwa wateja na wadau zinaofanyanao kazi. Kampuni ya usafirishaji ya ADL inasema mapato yake yameongezeka kutoka Sh4 bilioni mpaka Sh8 bilioni ndani ya miaka mitatu iliyopita yakichangiwa na ushiriki wake kwenye mashindano hayo.

Kama kuna kampuni inaweza kujivunia mafanikio ya kutokana na kushiriki mashindano ya Top 100 ya kampuni ndogo na za ukubwa wa kati, basi ni ADL Logistics.

ADL, kampuni inayojihusisha na biashara ya usafirishaji vifurushi, ilishika nafasi ya 40 wakati mashindano hayo yalipoanza mwaka 2011, lakini haikukata tamaa.

Badala yake ADL, ambayo ni kampuni tanzu ya Freight In Time (FIT), ilitafakari na kuongeza umakini kwenye shughuli zake.

Kwa kutambua umuhimu wa jukwaa hilo, mwaka 2016 ADL ilishika nafasi ya pili hivyo kujiongezea uaminifu miongoni mwa wateja inaowahudumia, suala ambalo ADL inasema lilichangia biashara yake kukua.

“Mizigo tunayosafirisha imeongezeka kutoka vifurushi 24,000 mwaka 2016 hadi 40,000 mwaka jana, huku mapato yakikua kutoka Sh4 bilioni mpaka Sh8 bilioni katika kipindi hicho,” anasema Frederick Mlay, mkurugenzi mtendaji wa ADL.

Anasema kuna wawekezaji wengi wa ndani na nje ya nchi ambao wanataka kuanzisha viwanda, akisema wamekuw wakiulizia namna mizigo yao inavyoweza kusafirishwa.

Anasema ukuaji wa kampuni yao unategemea utekelezwaji wa mpango wa Serikali wa kuwa na uchumi wa viwanda ambao utazalisha bidhaa nyingi zitakazohitaji huduma yao ya usafirishaji.

“Nina imani mpango huo utakuza biashara kwa kiasi kikubwa kwani wanaofungua viwanda wanahitaji kuzisafirisha ziwafikie wateja waliopo kote nchini,” anasema.

Kutokana na mwenendo huo, Mlay anasema mwakani wanatarajia kufungua ofisi ndogo katika mikoa ya Mbeya, Kigoma na Mwanza, mpango utakaogharimu Sh183 milioni ili kusogeza huduma kwa nchi jirani.

Mkurugenzi huyo anasema Top 100 imeipa kampuni yao fursa ya kukutana na wateja wapya hivyo kuongeza ufanisi wa biashara.

Licha ya kukuza biashara na kuongeza mapato, kampuni hiyo pia imeongeza uwezo wake wa kukabili changamoto zilizopo sokoni au mabadiliko ya mwenendo wa uchumi kama lilivyokuwa anguko la biashara mwaka 2017 lililoziathiri kampuni nyingi za usafirishaji ikiwamo ADL.

Kutikisika kwa biashara hasa ya usafirishaji kulisababishwa na baadhi ya wafanyabiashara kutoka Jamuhuri ya Kideokrasia ya Kongo (DRC) na Zambia kupungua kutumia bandari ya Dar es Salaam kwa sababu mbalimbali.

“Serikali imeshakaa na hizo nchi na wametatua changamoto zilizokuwapo na kuondoa vikwazo vilivyojitokeza hata kuwazuia wafanyabiashara hao kutumia bandari ya Dar. Sasa wateja wamerejea upya biashara inakwenda vizuri,” anasema Mlay.

Awali, anasema ADL ilikuwa inatafuta jukwaa la kujitangaza ndipo wakatapa mashindano ya Top 100 ambayo yamekuwa msaada mkubwa kwao tangu walipoanza kushiriki.

Kwa uzoefu waloupata, kampuni hiyo inapendekeza Top 100 iendelee kwakuwa inasaidia kuwafungua watu kifikra na kuwasaidia kutangaza biashara zao hususan kampuni za kati.

Muda mfupi baada ya kampuni hiyo kushiriki mashindano ya Top 100, Mlay anasema ilikua kwa asilimia 19 na imeendelea kustawi kila mara. Anashauri, kampuni yoyote ya kati inayohitaji ustawi wake uwe imara basi mashindano ya Top 100 ndilo daraja sahihi.

Shindano la Top 100 huzihusisha kampuni zenye mauzo ya kuanzia Sh1 bilioni hadi Sh20 bilioni kwa mwaka na huratibiwa na kampuni ya ukaguzi wa hesabu za fedha ya KPMG ikishirikiana na Mwananchi Communications Limited (MCL), wachapishaji wa magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti.

Mwaka huu, shindano hilo linatarajiwa kufanyika Alhamisi ya wiki ijayo likidhaminiwa na Benki ya NMB, Hoteli ya Hyatt Regency, Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na Azam Tv.

Mipango ya FIT

Ikiwa na uzoefu wa miaka 20 katika biashara ya usafirishaji wa shehena na vifurushi, kampun ya FIT inapatikana katika nchi nane barani Afrika.

Ukiacha Tanzania, kwa sasa FIT inapatikana Kenya, Uganda, Ethiopia, Sudan Kusini, Rwanda, Burundi na Djibouti lakini kutokana na kuendelea kukua, inatarajia kujitanua zaidi ya hapo ilipofika.

Ushiriki wao katika mashindano ya Top 100 ni miongoni mwa nyenzo muhimu ya kufanikisha mkakati huo wa kufikisha shughuli zao kwa wateja wengi zaidi.

“Shindano la Top 100 limetusaidia mambo mengi ikiwamo kupata mikataba ya kibiashara na baadhi ya kampuni kubwa duniani zinazofanya usafirishaji wa mizigo hasa kwa kutumia meli pamoja na kuaminiwa na wateja,” anasema Mlay.

Kutokana na kuongezeka kwa wateja na kukua kwa biashara, mwaka ujao ADL inatarajia kukua kwa asilimia 21.

Kwa mujibu wa Mlay kabla hawajashiriki Top 100 kampuni yao ilikuwa na wafanyakazi 20 tu lakini sasa hivi wamefika 70 huku kukiwa na mpango wa kuongeza zaidi idadi hiyo.

Changamoto

Sekta ya usafirishaji bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo wateja kutofikishiwa mizigo yao kwa wakati kutokana na mamlaka mbalimbali za usimamizi zilizopo katika maeneo mbalimbali.

Mlay anatolea mfano wa Dubai ambako utaratibu mzima wa kushughulikia vibali vya mzigo huchukua siku moja lakini nchini ni siku nyingi zaidi.

Anasema kituo cha pamoja cha forodha ni muhimu kusaidia kuondoa kikwazo hicho kwani mambo yote yatakuwa yanakamilika kwa siku moja kwakuwa maofisa wa mamlaka tofauti wanakuwa chini ya mwamvuli mmoja.