AG aunganishwa kesi ya Mbowe, DC Hai

Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG),George Masaju

Muktasari:

Kesi hiyo ilifunguliwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Kilimanjaro Veggie Limited (KVL), Freeman Mbowe, akimtuhumu mkuu wa wilaya kuharibu miundombinu ya shamba lake.

Moshi. Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), ameingia kwenye kumbukumbu za mwenendo wa shauri la madai ya fidia ya Sh549 milioni, dhidi ya Mkuu wa Wilaya ya Hai, Gelasius Byakanwa baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Moshi kuombwa aunganishwe kwenye kesi hiyo.

Kesi hiyo ilifunguliwa na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Kampuni ya Kilimanjaro Veggie Limited (KVL), Freeman Mbowe, akimtuhumu mkuu wa wilaya kuharibu miundombinu ya shamba lake.

Julai 13 mwaka huu, Byakanwa kupitia kwa wakili wake, Modestus Njau aliiomba Mahakama iruhusu AG aunganishwe katika kesi hiyo, akisema hawezi kushtakiwa peke yake.

Kwa mujibu wa maelezo ya wakili huyo, yeye (Byakanwa), alikuwa akitekeleza wajibu wake na sio mtu binafsi kama ambavyo ameshtakiwa.

Kabla ya kuanza kwa kesi hiyo jana, Mwanasheria wa Serikali Kanda ya Moshi, Kassim Nassir alijitokeza na kutaka aingizwe kwenye kumbukumbu za Mahakama akisema anamwakilisha AG.

Wakili Nassir alisisitiza uwapo wa AG kwa jana uwe katika kumbukumbu za mwenendo wa kesi hiyo na kwamba Naibu Msajili alirekodi uwapo wa AG katika shauri hilo.

Katika hati ya madai iliyowasilishwa mahakamani na Wakili D’Souza wa Jijini Arusha, Mbowe analalamikia kitendo cha Byakanwa kuingia kwa jinai katika shamba lake na kufanya uharibi huo.

Pia anadai Byakanwa hakuwa na mamlaka ya kisheria kufanya alichokifanya na kuiomba Mahakama itoe zuio la kudumu kwa Byakanwa kutoingilia shughuli za KVL.