Friday, November 3, 2017

Abiria Qatar Airways walambishwa dume

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

 Wakati likisherehekea miaka 20 ya utoaji wa huduma, Shirika la Ndege la Qatar limetangaza punguzo la bei kwa tiketi zitakazodumu kwa mwaka mzima.

Kuanzia Novemba mosi mpaka 10, wateja 20 wa shirika hilo wanaweza kushinda tiketi za daraja la tatu (economy class) na la pili (business class) zenye punguzo hilo ambazo wanaweza wakazitumia kati ya Novemba mosi hadi Oktoba 31, 2018.

Ofisa mkuu wa biashara wa shirika hilo, Ehab Amin alisema kwenye promosheni hiyo abiria wa daraja la pili anaweza kushinda tiketi mbili akilipia moja wakati wa yule wa lile la kwanza akipata tatu iwapo atalipia mbili.

“Huu ni mwaka maalumu wa kuwaleta karibu wateja wetu kuwashirikisha kwenye maadhimisho haya muhimu. Abiria wetu kutoka popote duniani wanaweza kushiriki shindano hili wanapoandaa safari zao kuelekea watakako kati ya vituo vyetu 150 vilivyopo,” alisema ofisa huyo.

Licha ya tiketi hizo zenye punguzo la mpaka asilimia 50, abiria wa Qatar iliyopata tuzo ya shirika bora la ndege zinazotolewa na Skytrax mwaka huu, wanaweza kujishindia uanachama wa wateja maalumu (privilege club gold) waliosambaa duniani kote.

Mwaka huu pekee shirika hilo linalokua kwa kasi lenye zaidi ya ndege 200 zimeanza kutua Auckland (New Zealand), Dublin (Ireland), Nice (Ufaransa) na Prague (Jamhuri ya Czechoslovakia) huku likipanga kufanya hivyo Canberra (Australia), St Petersburg (Urusi) na Cardiff (Uingereza) mwakani.

Kwa mujibu wa shirika hilo, limejitanabaisha kuwa miongoni mwa mashirika yasiyovumilia usafirishaji haramu wa wanyamapori.

Usafirishaji wa wanyamapori duniani ni biashara haramu ya nne kwa ukubwa ikiwa inakadiriwa kuwa na thamani ya Dola 19 bilioni za Marekani (zaidi ya Sh42 trilioni) kwa mwaka.

Biashara ya wanyama na mimea iliyo hatarini kutoweka inachochewa na mahitaji ya vito, mapambo na matibabu yasiyothibitika na ina madhara makubwa kwa uhifadhi wa kimataifa.

-->