Abiria mwendokasi wateseka na kadi

Muktasari:

  • Kadi hizo hazipo kwenye vituo vya mabasi hayo muda mrefu sasa, jambo ambalo linachangia kuongezeka kwa foleni kwenye vituo wakati wa ukataji tiketi.

Dar es Salaam. Msururu wa abiria kwenye mabasi ya mwendokasi, umesababishwa na ukosefu wa kadi za malipo za mabasi hayo, imeleezwa.

Kadi hizo hazipo kwenye vituo vya mabasi hayo muda mrefu sasa, jambo ambalo linachangia kuongezeka kwa foleni kwenye vituo wakati wa ukataji tiketi.

Akizungumzia suala hilo jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart), Mhandisi Ronald Rwakatare alikiri ukosefu wa kadi hizo kwenye vituo.

Rwakatare alisema mchakato wa kumtafuta mzabuni ambaye atakabidhiwa kusimamia utengenezaji wa kadi kwa sasa umesimama.

“Nashindwa kuongelea zaidi jambo hili kutokana na unyeti wake, kwa sababu umeunganishwa na mfumo wa kielektroniki na ule wa kibenki,” alisema Rwakatare.

Alieleza kuwa lengo lao ni kupata kampuni ambayo itakapokabidhiwa mradi huo, itaweza kutolea majibu linapotokea tatizo lolote.

“Tunaomba radhi kwa ucheleweshwaji upatikanaji wa kadi hizo, kwa kuwa ni jambo nyeti linalohusisha suala la mambo ya fedha,” alisema Rwakatare.

Pia, alisema wapo kwenye uchunguzi kubaini sababu za idadi ya kadi zilizouzwa, ni robo tu zinatumika hadi sasa.

Naye Ofisa Mkuu wa Operesheni Kampuni ya Max Malipo, Ahmed Lussasi alisema awali walishinda zabuni na kupewa kazi ya kutengeneza kadi hizo, kadi 200,000 zilitengenezwa ila mradi huo haukufika mwisho na hivi sasa upo mikononi mwa Dart wenyewe.

Ongezeko la abiria

Tangu kuanza kwa mradi wa mabasi yaendayo haraka (BRT) idadi ya abiri imekuwa ikiongezeka na hadi Juni, ulikuwa unasafirisha watu 200,000 kwa siku kutoka watu 50,000 waliokuwa wakisafirisha mwaka jana baada ya mradi huo kuanza kazi.

Kuongezeka kwa idadi hiyo inaelezwa kuwa ni ishara ya wananchi kuukubali mradi huo na kuutumia kila siku, wanapokwenda na kurudi makazini.

Mradi huo unaendeshwa kwa ubia wa Dart, Kampuni ya UdaRT ambayo ndiyo inaendesha mabasi na Benki ya NMB ambayo inasimamia upatikanaji wa fedha za mradi huo. Pia, Maxcom Africa walikuwa wanaendesha mifumo ya kukusanya nauli.

Pia, mradi huo ambao bado upo kwenye majaribio, unaelezwa wakati mchakato wa kupanua njia za BRT ili watu wengi zaidi waweze kunufaika utakapomilika, idadi ya abiria inaweza kuongezeka maradufu.

Hata hivyo, mabasi hayo yamekuwa yakipata changamoto ya foleni kwenye makutano ya barabara, Rais John Magufuli aliahidi kuitatua kwa kujenga barabara za juu.

Tayari, ujenzi wa barabara hizo unaendelea makutano ya Barabara ya Mandela na Nyerere eneo la Tazara na Morogoro na Mandela/Sam Nujoma eneo la Ubungo.