Abiria wa mabasi watakiwa kununua tiketi kielektroniki

Muktasari:

Chama cha abiria kimekuwa mstari wa mbele kuwaelimisha abiria na kutaka mfumo wa kielektroniki utumike ili kuwaepusha abiria na mfumo wa kihuni unaoendeshwa na madalali wa tiketi.

Dar es Salaam.Chama cha Kutetea Abiria Tanzania (Chakua), kimeiomba Serikali kuwapa maelekezo wamiliki wa mabasi ya abiria kote nchini kuingia katika mfumo wa kielektroniki katika ukataji wa tiketi.

Mwenyekiti wa Chakua Taifa, Hassan Mchajama, amesema hayo jijini Dar es Salaam, leo Julai 21 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu alichokiita kusuasua kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kutekeleza mpango huo ili kuondoa kero katika sekta ya usafirishaji abiria nchini kwa kuondoa ulanguzi na udalali wa tiketi.

“Tumepeleka malalamiko yetu kwa Serikali na mamlaka husika (TRA) lakini hakuna jitihada za dhati ambazo zimewahi kuchukuliwa kumwondolea abiria kero hizo,” amesema Mchajama

Amesema wamekuwa mstari wa mbele kuelimisha umma (abiria) na kuzungumza na mamlaka husika nje na ndani ya sekta ya usafirishaji nchini juu ya umuhimu wa kuwa na mfumo bora wa utoaji huduma likiwemo suala zima la ukataji tiketi za mabasi kupitia mifumo ya kisasa ya kielektroniki.

Amesema kitu kimoja kinachoitia aibu sekta nzima ya usafirishaji abiria kwa nji ya mabasi hapa nchini ni mfumo mbovu na wa kihuni wa ukatishaji tiketi za mabasi ya abiria waendao mikoani.