Abiria wa mwendokasi wagombea kupanda magari

Muktasari:

Abiria wamesema sababu ni kuchelewa kwa magari kufika kituoni.

Dar es Salaam. Usafiri katika kituo cha mabasi yaendayo haraka cha Gerezani umekuwa wa kugombea kutokana na abiria kuwa wengi.

Mkazi wa Kimara, Janeth Goefrey amesema hali hiyo imesababishwa na magari kuchelewa kufika kituoni hapo.

Amesema baadhi ya abiria husubiri magari yasiyosimama vituo vingi yanayoelekea Kimara.

“Haya yaliyoandikwa express wengi wanayapenda ndiyo maana unaona wanagombea, yanakuwa na vituo vichache mnawahi kufika,” amesema Goefrey.

Abiria wengine wamesema magari yamekuwa hayafiki kwa muda na kusababisha abiria kuwa wengi, hivyo kuingia ndani kwa kusukumana.

Mwandishi wa Mwananchi ameshuhudia abiria wa magari yanayoelekea Ubungo Maji, Ubungo Terminal na Morocco wakiingia kwa kugombea.