Adai washtakiwa waliua tembo

Muktasari:

 Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Matiko alidai kuwa  Oktoba 28, 2012 alikwenda Kituo cha Polisi Oysterbay kutambua nyara za Serikali zilizokamatwa Kimara baada ya kupewa maelekezo na bosi wake.

Dar es Salaam. Ofisa wa Idara ya Wanyamapori wa Kikosi cha Kuzuia Ujangili Kanda ya Mashariki na Pwani, Hemed Matiko ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba tembo 93 waliuawa kutokana na meno waliyokamatwa nayo washtakiwa.

Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Matiko alidai kuwa  Oktoba 28, 2012 alikwenda Kituo cha Polisi Oysterbay kutambua nyara za Serikali zilizokamatwa Kimara baada ya kupewa maelekezo na bosi wake.

Akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Serikali, Paul Kadushi alidai nje ya kituo hicho cha polisi kulikuwa na gari lenye nyara hizo alizozitambua na kubaini ni meno 210 ya tembo, mifupa mitano na bendera moja ya Taifa.

Washtakiwa Peter Kabi, Leonidia Kabi na Charles Wainaina wanadaiwa kuwa Oktoba 27, 2012 katika eneo la Kimara Stop Over, Dar es Salaam walifanya vitendo vya uhalifu kwa kupanga, kukusanya na kuuza  vipande 210 vya meno ya tembo na vipande vitano vya mifupa ya mnyama huyo.