Adaiwa kukutwa na mihuri ya Serikali

Muktasari:

Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Lazaro Mambosasa amesema Machi 13 saa 10:30 jioni baada ya kupata taarifa walikwenda kufanya upekuzi kwenye nyumba ya mtuhumiwa huyo

Dar es salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linamshikilia mkazi wa Yombo Kilakala kwa tuhuma za kukutwa na nyaraka mbalimbali ikiwamo mihuri na vyeti vya taasisi za Serikali.

Akizungumza leo Machi 16 Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum Lazaro Mambosasa amesema Machi 13 saa 10:30 jioni baada ya kupata taarifa walikwenda kufanya upekuzi kwenye nyumba ya mtuhumiwa huyo kwa kushirikiana na uongozi wa Serikali ya mtaa na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa na nyaraka hizo.

“Baada ya kufanya upekuzi tulikamata mihuri ya Baraza la Mitihani (Necta), muhuri wa Veta (Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi Tanzania), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Sokoine (Sua), Chuo cha Bandari na Chuo cha Usafirishaji (NIT),” amesema Mambosasa.

Alitaja vitu vingine alivyokuta navyo kuwa ni mihuri ya Mahakama ya Kisutu, Mkuu wa Shule ya Marangu, Mkurugenzi wa Jiji la Estern London pamoja na nyaraka nyingine za shule za msingi na sekondari.