Ashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kulawiti

Muktasari:

Mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya wananchi wenye hasira kali kumkamata, kumpiga na baadaye kumfikisha katika kutuo kidogo cha polisi Shirimatunda

Moshi.Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro linamshikilia Wilson Kalanga (28) Mkazi wa Shirimatunda kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wa mdogo wake mwenye umri wa miaka sita.

Kamanda wa polisi mkoani hapa, Hamis Issa amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa baada ya wananchi wenye hasira kali kumkamata, kumpiga na baadaye kumfikisha katika kutuo kidogo cha polisi Shirimatunda.

Akizungumza na gazeti hili nyumbani kwao, mtoto huyo (jina limehifadhiwa) aliliambia Mwananchi kuwa Januari 8 majira ya saa tano asubuhi mtuhumiwa alimwita chumbani kwake lakini alikataa.

"Ba mdogo Wilee alikuja akaniita lakini mimi nilimkatalia, alinibembeleza na kuniambia njoo na nilipozidi kukataa alinishika kwa nguvu na kuniingiza ndani kwake na kunivua kaptula huku akiwa ameniziba mdomo na kunipaka mafuta kisha kunifanyia unyama huo," amesema mtoto huyo

"Nilijiskia maumivu makali na kila nilipojaribu kupiga kelele nilishindwa hadi alipomaliza na kuniambia kuwa nisemwambie  mama atanipa hela."

Amesema alipomaliza kumfanyia unyama huo alitokea mama yake na kupiga kelele ndipo mtuhumiwa huyo alipotoka nje na kukimbia.

Kwa upande wake mama mzazi wa mtoto huyo ameliambia Mwananchi kuwa mara baada ya kumkuta shemeji yake akimfanyia mtoto wake kitendo hicho  alipiga kelele za kuomba msaada wakati huo shemeji yake alikua ameshakimbia.

"Nilishtuka sana kumuona shemeji yangu akimfanyia mwanangu kitendo kile kwani ni sawa na mtoto wake, nilimchukua mwanangu na kwenda naye polisi ili tupewe fomu namba tatu kisha twende hospitalini," amesema

Alisema mara baada ya kufika kituo cha Polisi cha Shirimatunda na askari aliyekuwepo zamu kumuona mtoto akiwa na mbegu za kiume na kinyesi, alimwandikia fomu hiyo kwa ajili ya kwenda hospitalini.

"Tulifika hospitalini na kupokelewa, sasa wakati tukiwa pale alikuja bibi yake na mwanangu na dada yake na mtuhumiwa waliingia chumba cha kwanza wakiwa na mwanangu na kutoka nje huku wakidai chumba hicho hakikuwa na kitanda," amesema mama wa mtoto huyo

Amesema kilichomshangaza ni kitendo cha kuingia tena kwenye chumba kingine na ndipo daktari akasema mtoto hajafanyiwa kitu na yupo salama huku mama mkwe wake akimtaka suala hilo likamalizwe kifamilia.