Adaiwa kumnywesha mkojo mtoto

Picha File

Muktasari:

Mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika

Mwanza. Mkazi wa Mtaa wa Shede wilayani Nyamagana mkoani hapa anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumnywesha mkojo mtoto wake wa kambo mwenye miaka tisa (jina linahifadhiwa) ikiwa ni adhabu ya kujisaidia haja ndogo kitandani akiwa usingizini.

Mtoto huyo anayesoma darasa la tatu katika moja ya shule za msingi jijini hapa, alipewa adhabu hiyo Mei 23 mwaka huu.

Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mwanza, Bethnsimbo Shija alisema mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa awali kukamilika.

Aliwaomba wananchi kutoa taarifa polisi na mamlaka nyingine za dola kwa watu wanaofanya unyanyasaji ili kudhibiti vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.

Mtetezi wa Haki za Watoto kutoka Taasisi ya Foundation Karibu Tanzania (FKT), Frank Benjamini alisema alipokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa mwalimu wa darasa wa mtoto huyo ndipo alipofungua jalada polisi na kufanikisha mtuhumiwa kutiwa mbaroni.

Mama mzazi wa mtoto huyo, Jessica Joseph ambaye hivi sasa yuko kwenye ndoa nyingine baada ya kutengana mumewe wa awali, alisema ameamua kumchukua mtoto wake na kuishi naye kutokana na kuhofia kutendewa ukatili zaidi. “Wakati mamlaka husika zikiendelea kuchukua hatua za kisheria, nitamchukua na kuishi na mwanangu asije akakutwa na makubwa zaidi; nitawasilisha maombi rasmi ya kupewa haki ya kukaa na mtoto wangu badala ya kuishi na mama wa kambo,” alisema Joseph.

Mwalimu mkuu wa shule anayosoma mtoto huyo, Valentina Rugera alisema kwamba uongozi wa shule ulilazimika kuwasilisha suala hilo ofisi za FKT.