Afande Sele katikati ya vibaka Tandika

Afande Sele

Muktasari:

Anachati tu muda wote mpaka anasahau rasta zake zimekaaje kichwani.


Seleman Msindi kwenye utawala wake Bongo Fleva ikitii maagizo yake kutoka mitaa ya Misufini kule Morogoro. Ana simu mpya aina Nokia kioo kipana kama ‘pichi’ ya Uwanja wa Uhuru. Simu yenye hadhi ya Afande Sele na mamlaka ya Ufalme wa Rhymes.

Anachati tu muda wote mpaka anasahau rasta zake zimekaaje kichwani. Wakati huo ni mwendo wa ujumbe mfupi na kupiga simu tu. Hakuna whatsApp wala instagram. Yuko busy kujibishana na washikaji na mshabiki kwa meseji.

Anaendeshwa na dereva wake yeye yupo upande wa kushoto, kioo chini. Afande Sele tena. Hataki kiyoyozi ili asionekane anaringa kwa mashabiki wale wa kupunga mikono na kutoa tano kwa Mfalme wa Moro. Hana habari Dar es Salaam yote yake, Temeke inamtii. Mfalme anapita watu waliimba jina lake.

Kila mmoja alimuita anavyotaka. Baba Tunda. Mfalme. Wale wa kumuita Rasta. Masela waliishia kuita Afande. Wazee na kina mama walimuita Msindi. Na wale waliomfahamu toka kitambo walifupisha kwa kumuita Sele.

Majina yote yalikuwa maarufu kama lilivyo jina lake la kisanii la Afande Sele. Mikono yake ilikuwa na usugu siyo kwa sababu ya kupiga push up. Hapana, ila ni kitendo cha kutoa tano kila sekunde kwa mashabiki na washikaji kila apitapo.

Ni mida ya jioni kama saa moja. Anga la Jiji la Marehemu Abbas Kandoro kwa wakati huo, limefifia kwa ujio wa giza linaloruhusu maasi yaendelee bila kificho. Giza linalozalisha kila aina ya dhambi mitaani. Wezi. Vibaka. Malaya. Na walevi wa kutosha.

Ni wakati ambao binadamu wapenda starehe wanaamka kwenda maeneo yao. Ni muda mzuri wa kuijua sura halisi ya jiji na wakazi wa Dar es Salaam. Wazee kwa vijana wapo katika harakati za starehe. Muda ambao kama hujaingiza kitu mfukoni utajiona mwenye mkosi.

Wapiga kinywaji wanatapakaa kwenye baa zisizo na idadi. Watu wa muziki katika kumbi za starehe. Wale wa sinema utapishana nao kwenye korido za Mlimani City, Dar Free Market nk, wakinukia marashi na uturi kama vile wametoa rushwa kwa Mungu kwamba wao hawatakufa milele amina.

Pia malaya ndo mida ambayo wamejipara tayari kuingia mzigoni.

Wakijiuza mitaani na kwenye baa. Wanapishana na majizi, majambazi, wezi wa wake/waume za watu, mafisadi ambao wametoka kazini na kuondoka na chochote kitu kwa kuiba, huo ndo muda wa matumizi.

Ni mitaa ya Tandika Afande Sele katoka Morogoro kuja Dar es Salaam, siyo kuja kula bata kama wakazi wa Jiji hili. Hapana, ni muendelezo wa shoo zake nyingi alizofanya kila siku. Wakati gari likikatiza kwa mwendo wa taratibu... Mara paap... simu haipo.

Kilichotokea ni kwamba lilikuwa tukio la ghafla kama video za GIF. Alishangaa mikono iko tupu bila simu. Kugeuka hivi hakuona kitu zaidi ya kivuli cha kijana ambaye kwa sekunde moja tu unatambua kuwa ni biandamu chakavu wa mavazi, afya na sura, akitokomea uchochoroni kwa spidi ya hatari.

Dereva wake hakuona lolote zaidi ya kusikia neno “we rudisha simu”.

Wakati anatoa neno hilo ilienda sambamba na tukio la Sele kuruka kupitia dirishani. Aliona kufungua mlango ni njia ndefu itamchelewesha kumuwahi kibaka.

Dereva alisikia kishindo nje ya gari, baada ya Sele kuruka kipitia dirishani.

Hakujali, na vumbi lake akainuka kwa kasi ya kutisha kumfukuzia kibaka ambaye muda huo alikuwa mtaa wa pili tayari. Ni siku ambayo iligundulika kuwa Sele ni mwanariadha pia.

Ieleweke kuwa kupoteza mawasiliano, angekosa pesa za shoo. Namba za mapromota, watangazaji, waandishi na wadau mbalimbali wa muziki aliokuwa anawasiliana nao. Bila simu asingejua ratiba ya studio kwa P Funk, wala siku ya kugonga ‘kopi’ kwa Mdosi pale Kariakoo.

Tandika vibaka ni wengi kuliko nguzo za umeme. Ni wengi kuliko nyumba zenye uzio (fensi). Kifupi katika watu kumi, nane kati yao ni vibaka. Ogopa. Halikuwa eneo rafiki kwa watumiaji wa simu na wadada wale wabeba mapochi makubwa kama majeneza.

Wakati anamkimbiza kibaka, alijua akienda kichwa kichwa anaweza kurudi na ‘boksa’ tu, maana mwizi alizidi kutokomea bondeni ndani ndani. Na yeye anachotaka ni simu na hata alikokuwa anaenda jioni hiyo bila simu isingekuwa na maana.

Akatumia akili ya kuzaliwa fasta huku akituma hatua kama Usain Bolt. Kawaida watu huwa wanaita “mwizi, mwizi, mwizi...” wanapofukuza kibaka, lakini yeye akawa akitaja jina lake “Mimi ni Afande Sele jamani. Mimi ni Afande Sele ndugu zangu. Mimi ni Afande Sele enyi Watanzania.” Hii ilimsaidia sana maana ni maeneo hatarishi.

Alifanya hivyo ili hata yule kibaka ikibidi kama ni shabiki wa muziki wa Sele arudishe simu, au akikutana na vibaka wengine wasimdhuru maana vibaka wana ushirikiano kama bodaboda kwenye shughuli zao za kiuchumi hatarishi.

Ni maeneo ambayo kama siyo mwenyeji huwezi kusogea hatua tatu mbele. Lakini kwa umuhimu wa mawasiliano Sele akakomaa. Sasa raia wakawa wanamshangaa yeye badala ya kusaidia kukamata mwizi.

Vibaka walizidi mno Tandika, matukio ya kupigwa mapanga. Kuporwa simu, nguo, au kufanyiwa vurugu. Ilikuwa ikishafika mida ya saa moja jioni huwezi kupita baadhi ya mitaa. Ni kama lilikuwa eneo lao la kujidai, sijui kwa sasa.

Ni kipindi ambacho kukatiza usiku maeneo yale ni sawa na kukatiza Mikumi usiku kwa miguu, halafu ulalamike simba wamezidi uroho. Maisha yamebadilika sana, leo hii watu wanaogopa simu kuishiwa chaji kuliko vibaka.

Mbinu ya Afande Sele ilimsaidia sana. Kwani alijikuta katikati ya masela kibao ambao walikuwa mafichoni kurutubisha akili zao za kihalifu kwa kubwia unga na bange. Walipomuona wakamsimamisha, wakati huo yule kibaka aliwapita hao masela kama roketi.

Kwanza walianza kumsifia Afande kwa uwezo wake wa kuandika mashairi yenye ujumbe mzito, huku wakisisitiza kuwa alistahili kuwa Mfalme wa Rhymes. Sifa ambazo zilitawala kwa muda mrefu na kusahau shida ya mwenzao ambayo ni simu.

Baada ya kupokea sifa zake Sele akajaribu kuwatuliza sasa ili awaeleze juu ya kuibiwa simu yake. Ajabu ni kwamba wale masela hawakuwa na wasiwasi juu ya hilo na kumuahidi kuwa arudi kesho atapata simu yake.

Alichoambiwa kwanza ni jina kamili la yule kibaka. Maana kila kibaka anajulikana maeneo yake ya kazi. Pia alihakikishiwa kuwa laini ya simu hatoipata ila simu ataipata maana huyo kibaka ni lazima atafika eneo lile kuripoti.

Aliporudi kesho yake mapema kabisa. Aliikuta simu yake nzima kwenye mikono salama lakini ikiwa haina laini kama walivyomuleza jana yake. Alichofanya ni kuwapoza kwa pesa kidogo kisha akaendelea na shughuli zake.

Nini maana yake? Maana yake ni kwamba hayo ndiyo matumizi sahihi ya umaarufu wa mtu kwa jamii. Lakini mastaa wa sasa wanaamini ustaa ni njia ya kurahisisha kupata madem au madanga kwa wale wa kike.

Mastaa wa sasa wanashindwa kutumia umaarufu wao kuijenga jamii, wao huona ufahari kuwa na mashabiki wengi mitandaoni. Badala ya kuwatumia hao mashabiki kutengeneza pesa halali. Wao wanawatumia kutengeneza vita ya chuki baina yao.

Kuna baadhi ya mastaa ni mfano mzuri kwa jamii. Na wanautendea haki umaarufu wao, lakini wengine wanaishia kufanya vijana wa kiume wapendeze kwenye mavazi ya kike.

Yaani watoto hawana kitu cha kuiga kwao zaidi ya mavazi ambayo hata malaika mbinguni wanashindwa kutambua ni kijana wa kiume au wa kike? Mastaa ni rahisi sana kuharibu jamii kwa tukio moja tu.

Vijana wengi hivi sasa wakipata umaarufu tu, tayari mavazi yao hayaeleweki, kujiremba watoto wa kiume, sijui kutengeneza nywele na hereni kama watoto wa kike. Athari zake zinakuja na ni mbaya sana kwa kizazi hiki.

Kitu kingine ni kiki ambazo kila mwanamuziki akitoa wimbo, huanza kuutangaza kijinga au kutupia mapicha ya ovyo ovyo mitandaoni na vitu kama hivyo.

Nyimbo nyingi wanazoimba zina ujumbe wa matusi ambao unaeleweka wazi kabisa. Na watoto wanazipenda na wanaelewa kabisa kwamba hili ni tusi.

Umaarufu kisiwe kijiwe cha maangamizi kwa jamii yetu kitabia. Umaarufu liwe daraja bora kati ya masikini, matajiri na watawala. Ukishakuwa maarufu tayari wewe unawakilisha wananchi kama Wabunge.

Kumbadilisha msanii wa Kitanzania ni tabu mno. Tatizo lao tayari huona wako sahihi kabla ya kusahihishwa. Na wana tabia za kidikteta kwamba kuwasahihisha ni kuwavunjia heshima zao.

Mafanikio bila umakini ni kitu kibaya, kwa sababu hufanya hata wale wenye elimu kubwa huamini hawawezi kushindwa. Kutoamini hilo ni sehemu ya wendawazimu. Ni sawa na mtu aliyekosa hofu.