Afariki dunia baada ya kuhukimwa jela maisha kwa kunajisi

Muktasari:

Akiwa kwenye chumba maalumu alianza kulalamika kuwa anajisikia maumivu makali na mwili kuishiwa nguvu

Chunya. Mkazi wa Matundasi, Godfrey Elikana (31), amefariki dunia katika hospitali ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kupatikana na kosa la kumnajisi mtoto wa miaka mitatu.

Tukio la kufariki kwa Godfrey limevuta hisia za watu wengi wilayani hapa huku baadhi wakidai alipata shinikizo la damu na wengine wakidhani ni kutokana na uwoga wa kufungwa jela.

Akizungumzia tukio hilo jana, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Dk Staford John alisema Godfrey alifikishwa hospitalini hapo usiku akiwa amezidiwa na kufariki dunia saa 12:00 asubuhi alipokuwa akiendelea kupatiwa matibabu.

Godfrey alihukumiwa kutumikia adhabu hiyo na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya, Osmund Ngatunga.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Ngatunga alisema aliridhika na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, ukiwamo wa daktari aliyemfanyia uchunguzi mtoto huyo na mshtakiwa alistahili kwenda jela maisha.

Awali, akitoa ushahidi mahakamani hapo, Dk Morris Mdoe wa hospitali hiyo, alidai kuwa aligundua mtoto huyo alinajisiwa baada ya kumkuta akiwa na michubuko kwenye sehemu ya haja kubwa.

Hata hivyo, baada ya mshtakiwa huyo kusomewa hukumu hiyo, aliondolewa kizimbani akiwa mzima na kupelekwa kwenye chumba maalumu mahakamani hapo kwa ajili ya kusubiri utaratibu wa kumsafirisha kwenda jijini Mbeya kuanza kutumikia kifungo gerezani.

Akiwa kwenye chumba hicho, mshtakiwa huyo alianza kulalamika kuwa anaishiwa nguvu na maumivu makali, jambo lililowafanya askari waliokuwa wakimlinda kumpeleka hospitali hiyo ya wilaya ambako alikumbwa na mauti.