Pacha walioungana waendelea na matibabu

Muktasari:

Wanasoma mwaka wa kwanza Chuo Katoliki cha Ruaha (Rucu).

Dar es Salaam.  Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) imesema afya ya pacha walioungana, Maria na Consolata Mwakikuti inazidi kuimarika.

Pacha hao wanaosoma mwaka wa kwanza Chuo Katoliki cha Ruaha (Rucu), walifikishwa JKCI  Januari 2,2018 baada ya kupewa rufaa kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, walikokuwa wamelazwa tangu Desemba 28, mwaka jana.

Akizungumza na MCL Digital leo Februari 5, 2018 ofisa uhusiano wa JKCI, Anna Nkinda amesema bado wanaendelea kupatiwa matibabu ya moyo.

"Maria na Consolata wapo kwenye uangalizi wa jopo la madaktari  bingwa sita na wanaendelea vizuri na matibabu. Kiutaratibu majibu ya mgonjwa ni siri kati yake na daktari,” amesema Anna.

Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI ambaye ndiye kiongozi wa jopo la madaktari wanaowatibu pacha hao, Profesa Mohamed Janabi amesema majibu ya pacha hao yatawasilishwa wizarani.

Pacha hao waliolelewa na Shirika la Masista la Maria Consolata tangu walipozaliwa mwaka 1996 hadi walipohitimu kidato cha sita, sasa wanahudumiwa na Rucu kwa kushirikiana na Serikali ya Mkoa wa Iringa.