Wabunge wahoji agizo la Rais Magufuli

Muktasari:

January Makamba amesema kwa eneo alilozungumzia Rais wataweka mwongozo wa matumizi yake kwa mujibu wa sheria.

Dar es Salaam. Agizo la Rais John Magufuli kuhusu wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka vyanzo vya maji wasibughudhiwe limeibua maswali bungeni ikielezwa Rais amevunja sheria.

Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa katika swali la nyongeza bungeni amesema, “Kwanza niipongeze wizara mara nyingi imejitahidi kuelimisha jamii itunze mazingira, lakini sisi kama wawakilishi wa wananchi tumsikilize Rais au waziri? mara nyingi tumeambiwa akisema Rais ni sheria jana amewaambia waingie kwenye mabonde walime mpaka mvua itakapowatoa,  lakini waziri unazuia.”

Akijibu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Kangi Lugola amesema Rais Magufuli hajavunja sheria kuagiza mamlaka zinazohusika na mazingira kuacha kuwabughudhi wananchi wanaolima pembezoni mwa mito.

Pia, ameonya viongozi wanaochochea wananchi kuvunja sheria na wananchi waliozoea kuzivunja akisema Serikali itapambana nao.

Lugola pamoja na waziri wa wizara hiyo, January Makamba leo Jumatano Novemba 8,2017 wamesema sheria inatoa mamlaka kwa waziri kutoa kibali kwa shughuli kufanyika katika maeneo hayo.

Waziri January amesema kutokana na maelekezo ya Rais Magufuli ya jana Jumanne Novemba 7,2017 kwa eneo mahsusi kwa mujibu wa sheria wataweka mwongozo wa matumizi.

Rais Magufuli alisema busara itumike wakati wa utekelezaji wa  sheria ya mazingira inayozuia shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka kwenye chanzo cha maji ili kuwaondolea  kero wakulima wanaojitafutia chakula na kipato cha kawaida kwa ajili ya familia zao.

“Ni vyema utekelezaji wa sheria ya mazingira ya mita 60 ilenge zaidi kubana wanaotumia maeneo ya maziwa na bahari na si wananchi wanaolima mazao ya  chakula ya muda mfupi kando mwa mito,” aliagiza.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa mwananchi aliyejitambulisha kwa jina moja la Roshi, mkazi wa Kyaka wilayani Missenyi aliyedai kuwa mazao ya  chakula yaliyokuwa kwenye shamba lake lililopo kando mwa  mto yalifyekwa na watu wa mazingira kwa madai kuwa yalilimwa ndani ya mita 60.

Rais Magufuli alisisitiza agizo hilo wilayani Karagwe na hata mjini  Bukoba akiagiza wananchi hao kuendelea na shughuli za kujiongezea kipato na wasiondolewe katika maeneo hayo.

Kuhusu wananchi wanaodaiwa kuvamia vyanzo vya maji, Rais aliagiza watu zaidi ya 200 wanaodaiwa kuvamia vyanzo vya maji watafutiwe maeneo mengine kwa sababu ni kosa la viongozi na mamlaka husika zilizozembea kuwazuia mapema kuingilia maeneo hayo.