Ahadi ya umeme kila kijiji yatajwa kuwaharibia wabunge kwenye uchaguzi

Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare akizungumza bungeni alipokuwa akichangia mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2018/2019, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Kauli hiyo imetolewa na mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema), Wilfred Lwakatare

 


Dodoma. Mbunge wa Bukoba Mjini (Chadema),  Wilfred Lwakatare amesema kauli ya Serikali ya kupeleka umeme kila kijiji ni ya uongo, itawaweka katika wakati mgumu wabunge kwenye chaguzi mbalimbali nchini.

Akizungumza jana Mei 24, 3018 katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2018/19,  Lwakatare amesema kauli hiyo haifanani na kasi ya usambazaji wa umeme vijijini kwa maelezo kuwa miradi mingi inapangwa kwa ajili ya chaguzi mbalimbali, kusababisha kutotekelezwa.

“Miradi mingi inapangwa kwa ajili ya uchaguzi. Haiwezi kutekelezekwa, ukimsikiliza waziri (Dk Medard Kalemani-Waziri wa Nishati) anavyozungumza kuwa kila kijiji kitapelekewa umeme si kweli. Hoja hii haitekelezeki  na  itatuweka pabaya tutakapoulizwa (na wananchi),” amesema.

“Ni vyema Serikali ikawaambia wananchi kuwa watachukua umeme mahali utakapopitishwa kuliko kusema watapeleka umeme kila kijiji. Kupeleka umeme kila kijiji hakutekelezeki ni uongo uliokubuhu.”