Thursday, July 19, 2018

Ajali iliyoua mwanafunzi ilivyoibua vurugu Tarime

 

By Waitara Meng’anyi, Mwananchi wmeng’anyi@mwananchi.co.tz

Tarime. Lydia Ryoba, mwanafunzi wa darasa la nne katika shule ya msingi Nyangoto amefariki dunia baada ya kugongwa na gari, tukio lililosababisha vurugu na watu wanne kujeruhiwa kwa risasi.

 

Tukio hilo limetokea leo Alhamisi Julai 19, 2018 katika kijiji cha Nyanotoka kata ya Matongo wilayani Tarime mkoani Mara.

 

Gari hilo linalodaiwa kuwa la polisi baada ya kumgonga mtoto huyo lilielekea katika mgodi wa North Mara, jambo lililowafanya wananachi kuvamia geti la kuingilia katika mgodi huo wakiwa na mwili wa mtoto huyo kuanzia saa 5 asubuhi hadi saa 10 jioni.

 

Polisi walifika eneo hilo na kuwatawanya wananchi hao na kuchukua mwili wa mtoto huyo.

 

“Watu wanne wamejeruhiwa kwa risasi na wamelazwa kituo cha afya Sungusungu hapa Nyamongo,” amesema mmoja wa wananchi kwa sharti la kutotajwa jina.

 

Akizungumza na MCL Digital kamanda wa Polisi Mkoa wa Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe amesema, “Ni sahihi, wazazi walitaka mgodi ukubali kulipa fidia ndio wakakubali kuchukua mwili wa mtoto wao. Tulikwenda nao hadi katika uongozi wa mgodi wakakubali kugharamia mazishi.”

 

“Mwili wa mtoto huyo uko chumba cha kuhifadhia maiti. Unajua wahuni walitaka mgodi utamke kiasi cha fedha watakazotoa, ila hali ni shwari kabisa.”

 

Mrimi Zabron, Katibu wa mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche amesema, “ilikuwa tukio baya lakini tayari kumetulia baada ya polisi kutumia nguvu kuchukua mwili wa mwanafunzi yule na kuondoka nao.

 

Wananchi walikuwa wanamtaka askari aliyemgonga mtoto ili achukuliwe hatua.” amesema Zabron.

 

Mwenyekiti wa kijiji cha Nyangoto, Emmanuel Ryoba amesema mara kwa mara magari ya doria yanagonga wananchi katika kijiji hicho.

 

“Mtoto huyu alikuwa akitoka kuchota maji, Serikali inapaswa kuchukua hatua maana matukio haya yamezidi kwa kweli, wananchi wangu wanagongwa sana,” amesema.


-->