Ajali yaua watu watano Geita

Muktasari:

Majeruhi watatu wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi

Geita. Watu watano wamefariki dunia na wengine 36 kujeruhiwa baada ya basi walilokuwa wakisafiria kutoka Mwanza kwenda Bukoba kupinduka.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Mponjoli Mwabulambo alisema ajali hiyo iliyohusisha basi la King Msukuma na gari ndogo aina ya Toyota Harrier ilitokea jana asubuhi eneo la Kasamwa wilayani hapa.

Kaimu Mganga Mfawidhi Hospitali ya Mkoa wa Geita, Dk Mazoea Fimbo alisema maiti za watu watano, wanawake wanne na mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi sita zimepokewa na kuhifadhiwa katika chumba cha maiti hospitalini hapo.

“Majeruhi watatu wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Bugando jijini Mwanza kwa matibabu zaidi kutokana na hali zao kuwa mbaya na kuhitaji huduma Maalum,” alisema Dk Fimbo.

Alisema jumla ya majeruhi 36, kati yao 18 wakiwa wanawake walipokewa na kutibiwa; 10 walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka baada ya hali zao kiafya kuridhisha huku 21 wakilazwa kwa matibabu zaidi.

Akizungumzia ajali hiyo, mkuu wa mkoa wa Geita, Robert Gabriel alisema kwa mujibu wa maelezo ya mashuhuda, ajali hiyo ilitokea baada ya basi kukosa mwelekeo na kulifuata gari dogo upande wa kulia mwa barabara na kuligonga ubavuni kabla ya magari yote mawili kupinduka.