Ajali za barabarani zaipasua kichwa Taasisi ya Mifupa

Muktasari:

Akizungumza na Mwananchi jana, daktari bingwa wa upasuaji wa Mifupa na Magonjwa ya Ajali wa Moi, Kennedy Nchimbi alisema kwa siku chache zilizopita kumekuwapo na ongezeko kubwa.

Dar es Salaam. Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (Moi), imesema idadi ya majeruhi wanaofika kutibiwa katika kitengo cha dharura baada ya kupata ajali imeongezeka hadi kufikia wastani wa watu 30 kwa siku.
Akizungumza na Mwananchi jana, daktari bingwa wa upasuaji wa Mifupa na Magonjwa ya Ajali wa Moi, Kennedy Nchimbi alisema kwa siku chache zilizopita kumekuwapo na ongezeko kubwa.
“Ukiangalia kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita, Aprili tuliwapokea wagonjwa 650, Mei 435 na Juni tulipofunga mwaka tuliwatibu 693. Ni ongezeko kubwa ukilinganisha na miezi iliyopita na ni wastani wa wagonjwa 17 mpaka 30 kwa siku,” alisema Dk Nchimbi.
 Alisema mwaka 2016/2017 majeruhi wa ajali waliongezeka kutoka 6,669 hadi 8,283 kwa kipindi cha 2017/2018.
Dk Nchimbi alisema huenda idadi hiyo ikaongezeka mwaka 2018/2019 iwapo umakini usipoangaliwa, kwa kuwa Julai pekee wamepokea idadi kubwa ya wagonjwa.

Meza za upasuaji
Daktari huyo alisema kwa kipindi cha Julai ongezeko la wagonjwa limeifanya taasisi hiyo kufunga meza za ziada za upasuaji ili kuwahudumia majeruhi wengi kwa wakati.
Alisema kwa wiki  iliyopita walipokea idadi kubwa ya majeruhi kutoka Dar es Salaam na mikoani ambapo kwa siku walipokea wahanga hadi 30 huku idadi kubwa wakihitaji upasuaji wa dharura.
“Kwa mfano wiki iliyopita kuanzia Jumatatu mpaka Jumapili tulikuwa ‘bize’ mpaka tulifungua meza nyingine za ziada. Kila siku tuna meza ya dharura, lakini wanapokuwa wengi tunaona tutachukua muda mrefu, kwa hiyo inabidi tuwabadilishe akishuka mtu hapo anapandishwa mwingine,” alisema.
Hata hivyo alisema mgonjwa anaweza kufika kwa wakati lakini akachelewa kufanyiwa upasuaji kutokana na idadi kubwa ya majeruhi.
“Kuna nyakati wagonjwa 12 wapo mlango wa chumba cha upasuaji wa dharura na Moi tuna timu za madaktari kuanzia anayekuona, atakayekuandaa, atakayeenda kukufanyia upasuaji. Inabidi hizi timu ziongezwe na meza zaidi zifunguliwe,” alisema Dk Nchimbi.
Wengi hawana ndugu
Ofisa uhusiano wa Moi, Patrick Mvungi alisema licha ya ongezeko hilo, taasisi hiyo inaelemewa na gharama kubwa za kuwahudumia majeruhi hao kwa kuwa wengi wao hawana ndugu.
Alisema majeruhi hasa wale wa bodaboda matibabu yao huchukua muda mrefu na wengi hawana ndugu, lakini baadhi yao hata marafiki ambao hujitokeza baadaye hupotea.
“Baadaye huwa tunawatangaza kwenye vyombo vya habari na ikitokea bahati mbaya wakafariki (dunia), ikiwa ndugu zake hawajapatikana tutafanya taratibu za mochwari mwili unatakiwa ukae kwa muda fulani na tutawasiliana na manispaa ambao watazika.”
Alisema wapo watu ambao hubaki na akiba kidogo ya fedha kwa ajili ya matibabu, lakini changamoto kubwa kwa majeruhi wengi wa ajali ni kutokuwa na bima za afya.
Mkazi wa jijini Dar es Salaam, Rajab Kaumba aliishauri Serikali kuanzisha mpango wa utoaji wa elimu kwa jamii itakayosaidia kupunza ajali nchini.
“Kukiwa na elimu kuanzia shuleni, ajali zitapungua,” alisema.