Ajinyonga nje ya msikiti

Muktasari:

  • Kamanda wa polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan alisema tukio hilo lilibainika wakati waumini walipofika msikitini saa 11:00 alfajiri kwa ajili ya swala ya Subhi.

Pemba. Katika hali isiyokuwa ya kawaida mkazi wa Ole Mchanga, Mkoa wa Kaskazini Pemba, Azani Abdallah Suleiman (28) amekutwa amejinyonga katika mti uliopo nje ya msikiti wa Machomane, wilayani Chackechake.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Sheikhan Mohamed Sheikhan alisema tukio hilo lilibainika wakati waumini walipofika msikitini saa 11:00 alfajiri kwa ajili ya swala ya Subhi.

Sheikhan alisema baada ya waumini hao kuingia msikitini waliona maiti ya kijana huyo ikining’inia juu ya mti ulio nje ya msikiti huo.

Alisema taarifa za awali zinaeleza kuwa kijana huyo alifika kwa babu yake mkazi wa Machomane, Chakechake na kufanya mazungumza kuhusu mipango yake ya kuoa.

“Tumeambiwa kwamba hakukuwa na maelewano mazuri na babu yake baada ya kumpa taarifa hiyo, ilipofika usiku alimtaka mjukuu wake huyo akapumzike lakini baadaye kijana huyo alikwenda kujinyonga,’’ aliongezea Sheikhan.

Aliitaka jamii hususan wazazi wawe na utaratibu wa kuzungumza lugha nzuri na watoto wao ili kuepusha matukio ya aina hiyo, kwa kuwa yanaweza kupata suluhu ili kuepusha madhara kama hayo.

Kamanda Sheikhan alisema baada ya kuitwa na waumini, polisi walichukua mwili wa marehemu na kuupeleka Hospitali ya Chakechake na kufanyiwa uchunguzi na kwamba, haukuwa na jeraha lolote linaloashiria kupigwa au kuteswa.