Friday, September 14, 2018

Akamatwa kwa kuwapa dawa za kulevya, kuwabaka wanawake

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Jonathan

Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Jonathan Shanna 

By Jesse Mikofu na Johari Shani, Mwananchi. mwananchipapers@mwananchi.co.tz.

Mwanza. Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia Kenned Obworo (35), kwa kujihusisha na vitendo vya kuwanywesha dawa za kulevya wanawake na kisha kuwabaka.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Septemba 14, Kamanda wa polisi mkoa wa Mwanza Jonathan Shanna amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa Mtaa wa Rufiji katika Hotel ya Jawita Septemba 11, mwaka huu saa mbili asubuhi.

Amesema katika uchunguzi wao polisi wamebaini kuwa mtuhumiwa huyo anawalaghai wanawake kwa kuwanunulia chakula na vinywaji kisha kuwawekea dawa zinazodhaniwa za kulevya ili awabake, kuwaibia fedha na simu za mkononi kwenye nyumba za kulala wageni ambazo anakuwa amekodisha.

Kamanda Shana amesema Septemba 12, saa 2:00 usiku katika hoteli ya Haven iliyopo Nyasaka wilayani Ilemela, mtuhumiwa alimchukua mwanamke mmoja akamnunulia Redbul kisha akamuwekea dawa hizo, baada ya kulewa alimuingiza kwenye chumba na kumbaka.

“Baada ya mtuhumiwa kukamatwa alikutwa akiwa na pakiti mbili za vidonge aina ya Lorivan 2, pakiti moja ilikuwa na vidonge 3, nyingine haina hata kimoja,” amesema Shanna.

Amesema tukio kama hilo lilitokea wilaya ya Magu Septemba 10, katika baa iitwayo Dear Sija Lodge.

Amesema kabla ya tukio hilo wanawake wanne walikutana na mtuhumiwa huyo katika bar ya Villa Park jijini Mwanza ambapo walimuomba awanunulie vinywaji na alifanya hivyo kisha wakapeana namba za simu na kuachana salama.

Amesema majira ya mchana wanawake wawili kati ya hao wanne, walimpigia simu wakakubaliana wakutane tena Villa Park na walipokutana waliafikiana waende Kisesa kwa kutumia gari la mmoja wa wanawake hao.

Kamanda alifafanua zaidi kuwa baada ya kufika katika baa hiyo ya Dear Sija waliagiza vinywaji kisha wanaume wawili akiwamo mtuhumiwa waliingia chumbani na kuwaingiza wanawake hao ambapo waliwalevya na kuwabaka kisha kuwaibia simu mbili za Sumsung na kuwaacha hawajitambui.

Baada ya kufanya upekuzi kwenye vyumba hivyo walikuta vidonge aina ya Lorenzepam na mtuhumiwa amekiri kufanya matukio kama hayo katika mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Mara, Arusha na Mwanza.

Amesema uchunguzi wa awali unaonyesh vidonge hivyo aina ya Lorivan 2 na Lorenzepam ni dawa zinazotumiwa kwa wagonjwa wa akili ili kuwapa uzingizi au kuwalevya wakati wa kupatiwa matibabu.

-->