Akaunti kuchangia waathirika ajali ya MV Nyerere hii hapa

Muktasari:

  • Hadi leo saa 12:00 jioni zaidi ya Sh170milioni zimetolewa na wadau mbalimbali, ikiwemo kampuni za simu za mkononi za Tigo na Vodacom

Dar es Salaam. Serikali imefungua akaunti kwa ajili ya kuweka fedha zinazotolewa na watu mbalimbali kuwasaidia waathirika wa ajali ya kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.

Akaunti hiyo ni  ‘Maafa MV Nyerere 31110057246 tawi la Benki ya NMB Kenyatta Mwanza’.

Wakati akaunti hiyo ikitangazwa leo, Kampuni ya simu za mkononi ya Vodacom imetoa Sh10milioni kusaidia waathirika hao huku kampuni ya simu za mkononi ya Tigo ikichangia Sh150.

Michango hiyo imetolewa leo jioni Septemba 22, 2018 katika kisiwa cha Ukara ilikozama meli hiyo juzi Septemba 20, 2018.

Pia, jumuiya ya Shia ya Aish Nashir kutoka Dar es Salaam wamechangia Sh10milioni na katoni 3,300 za maji huku mfanyabashara Azim Dewji akitoa Sh10 milioni na katoni 3,000 za maji.

Akizungumza na waandishi wa habari katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe mkoani Mwanza, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama amemtaka mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella kuhakikisha fedha zinazochangwa zinawafikia walengwa.

“Ofisi ya waziri mkuu itaikagua akaunti hiyo mara kwa mara kuhakikisha kuwa michango inawafikia walengwa,” amesema Mhagama.

“Kama itatumika kinyume na taratibu tutachukua sheria kama tulivyofanya kipindi kile yalivyotokea maafa kule Kagera.”

Amesema kazi ya Serikali ni kuratibu shughuli za maafa na kwa kuzingatia sheria.

“Jambo kubwa ambalo  tunalitekeleza tumeagiza kamati ya maafa ya Mkoa wa Mwanza kufungua akaunti kwa ajili ya maafa ili michango  yote itakayotolewa na wadau kuwekwa kwa pamoja,” amesema.

Amesema akaunti hiyo itasimamiwa na kuratibiwa na ofisi ya maafa ya mkuu wa Mkoa wa Mwanza.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, IsackKamwelwe amewashukuru wananchi pamoja na kampuni mbalimbali zilizotoa michango.