Akutwa na SMG, risasi 24, simu 19, laini 58

Picha na Maktaba.

Muktasari:

Kabla ya kuuawa katika majibizano ya risasi, mtuhumiwa huyo anadaiwa kukamatwa na bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 24, simu 19 zilizoporwa maeneo mbalimbali na laini za simu 58.

Mkazi wa Dar es Salaam, Robert Massawe (51) ambaye polisi wanadai ni mtuhumiwa hatari wa uporaji na mauaji ameuawa kwa kupigwa risasi na watu wanaodaiwa kuwa ni wenzake.

Kabla ya kuuawa katika majibizano ya risasi, mtuhumiwa huyo anadaiwa kukamatwa na bunduki aina ya SMG ikiwa na risasi 24, simu 19 zilizoporwa maeneo mbalimbali na laini za simu 58. Taarifa iliyotolewa jana na kamanda wa polisi mkoani Kilimanjaro, Hamisi Issah ilisema mtuhumiwa huyo aliuawa juzi saa tisa alfajiri wilayani Rombo na watu wanaodaiwa kuwa watuhumiwa wenzake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtuhumiwa huyo pamoja na mkewe walikamatwa jijini Dar es Salaam na baada ya kuhojiwa na polisi anadaiwa kueleza matukio mbalimbali ya ujambazi aliyoshiriki.

Kamanda Issah alisema baada ya kukamatwa jijini humo na kuwaeleza polisi ushiriki wake katika matukio mbalimbali ya ujambazi alikubali kuwaonyesha mahala alipoficha bunduki hiyo.

Polisi waliandamana naye chini ya ulinzi mkali hadi Moshi kwenye dampo lililopo karibu na kiwanda cha ngozi ambapo bunduki ilipatikana ikiwa imefukiwa ardhini ikiwa na risasi 24. “Muda wote alitoa ushirikiano mkubwa kwa polisi na alivyokuwa akisimulia matukio aliyoyafanya mwili unaweza kusisimka. Simu tatu kati ya 19 tumegundua ziliporwa hapa Moshi,” alisema.

Katika mahojiano hayo inadaiwa mtuhumiwa huyo aliwaeleza polisi juu ya mpango uliokuwapo wa kufanya tukio la ujambazi katika kijiji cha Chilio, kata ya Holili wilayani Rombo juzi alifajiri.“Akiwa chini ya ulinzi wa askari kanzu alikubali kuwapeleka polisi katika eneo hilo, sasa walipofika alipowaona wenzake alipiga kelele ya kuwajulisha wenzake kuwa polisi walikuwapo eneo hilo,” alisema.

Kamanda Issah alisema hali hiyo iliwafanya watuhumiwa wenzake kukimbia huku wakipiga risasi ovyo na baadhi zilimpiga Massawe mkono wa kushoto, mgongoni na mguuni na kufariki. “Tuonavyo sisi wale wenzake walikuwa na nia ya kupoteza ushahidi au kumpoteza mwenzao. Wahalifu ndio walimpiga risasi mwenzao na pale hata polisi wetu wangedhurika kama si kujihami,” alisema.

Kamanda Issah alisema kati ya simu 19 alizokutwa nazo, moja alikuwa nayo mkewe ambaye anashikiliwa Dar es Salaam.