Ali Choki alazwa Bugando

Ali Choki

Muktasari:

Meneja wake amesema amelazwa tangu juzi, Septemba 3. 

Mwanza. Mwanamuziki aliyewahi kutamba katika bendi ya Twanga Pepeta, Ali Choki ambaye kwa sasa ni mwenyeji wa jiji la Mwanza, amelazwa katika hospitali ya Rufaa ya Bugando.

Taarifa kutoka kwa meneja wa msanii huyo, Ramadhani Said katika mahojiano na MCL Digital leo Septemba 5, amesema msanii huyo amelazwa hospitalini hapo tangu juzi.

"Ni kweli Choki kwa sasa anasumbuliwa na maradhi ila mimi sina mamlaka ya kuyataja. Hiyo ni siri kati ya daktari na mhusika mwenyewe," amesema Saidi.

Meneja huyo amesema Choki amehamishia makazi yake mkoani Mwanza akifanya kazi kwenye kundi la burudani la Super Kamanyola linalofanyia shughuli zake eneo la Kirumba jijini Mwanza.

Hata hivyo, afisa habari wa Bugando, Lucy Mogelle amesema hana uhakika wa uwepo wa msanii huyo ila ameahidi kufuatilia.

"Nipo kwenye kikao, nikitoka nitakujulisha. Nipe muda kidogo,"' amesema Mogelle.