Alichoahidi Polepole akimnadi mgombea udiwani

Muktasari:

Mgombea udiwani amewasihi wananchi wamchague aweze kushirikiana kikamilifu na Serikali kuwaletea maendeleo

Polepole amewasihi wakazi wa kata ya Makanya wilayani Same mkoani Kilimanjaro kumchagua mgombea udiwani wa chama hicho, Amiri Mbwambo ili akawe kiunganishi sahihi kati yao na Serikali.

Polepole ametoa kauli hiyo leo Julai 22, 2018 katika Kijiji cha Makanya wakati wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo.

Kabla ya uchaguzi utakaofanyika Agosti 12, 2018 Mbwambo alikuwa diwani wa kata hiyo kwa tiketi ya Chadema kabla ya kujiuzulu na kujiunga na CCM.

Amesema maendeleo wilayani Same na meeneo mengine yanatokana na sera nzuri za Serikali ya CCM ambayo imekuwa ikitoa fedha za kutekeleza miradi ya maendeleo.

Polepole amesema wananchi wanapaswa kuamka na kumchagua diwani anayetokana na CCM akashirikiane na Serikali.

Amesema endapo atachaguliwa Mbwambo, watakarabati barabara ya Makanya hadi Changoko yenye urefu wa kilomita 13 ambayo ni kiungo cha maendeleo ya wakazi wa kata ya Makanya na Same kwa jumla.

Amesema pia watahakikisha wananchi wa kata hiyo  wanapata huduma ya maji safi na salama na kuboresha shule kwa kujenga madarasa.

Mgombea Mbwambo amewasihi wananchi wa kata hiyo wamchague aweze kushirikiana kikamilifu na Serikali kuwaletea maendeleo.

Amesema akiwa Chadema alishindwa kutekeleza ahadi kutokana na kukosa kiungo serikalini, hivyo akichaguliwa sasa ana uhakika wa kuzitekeleza na kuboresha maisha ya wananchi.

Amesema atashirikiana na Serikali kuboresha miundombinu ya barabara, maji na kuanzisha elimu ya kidato cha tano na sita katika kata hiyo.

"Naomba mniamini kwa mara nyingine na mnipe nafasi ili niwatumikie, ahadi nilizozitoa nitazitekeleza kwa ukamilifu," amesema.

Mbunge wa Same Magharibi (CCM), Dk David Mathayo amesema tangu uchaguzi mkuu wa 2015 umalizike amepata wakati mgumu wa kuhudumia kata ya Makanya kutokana na kukosa wa kushirikiana naye.

Katika mkutano huo, wanachama sita wa Chadema akiwemo aliyewahi kuwa katibu wa Wilaya ya Same, Said Mwarabu walijiunga na CCM.