Alichokisema Makamba kuhusu mawasiliano yake na Mo

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), : January Makamba,

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), : January Makamba,  amezungumzia jinsi alivyokuwa mtu wa kwanza kupata taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’, akibainisha kuwa taarifa hizo alizipata kutoka kwa baba wa bilionea huyo, Gullam Hussein

Dar es Salaam. Unajua alichokisema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba baada ya kuulizwa sababu za kuwa wa kwanza kujua taarifa za kupatikana kwa mfanyabiashara Mohammed Dewji ‘Mo’.

Makamba alikuwa wa kwanza kuposti katika Twitter taarifa za kupatikana kwa bilionea huyo aliyetekwa Oktoba 11, 2018.

Mo alitekwa katika Hoteli ya Colosseum alikokwenda kufanya mazoezi na alipatikana Oktoba 20, 2018 baada ya watekaji kumtelekeza katika viwanja vya Gymkhana ambako alitembea umbali mfupi na kuomba  msaada wa simu na kuwasiliana na baba yake, Gullam Hussein.

Katika Twitter Makamba aliandika, “Mohammed Dewji amerudi nyumbani salama. Nimezungumza naye kwa simu dakika 20 zilizopita. Sauti yake inaonyesha yu mzima bukheri wa afya. Shukrani kwa wote kwa dua na sala. Naenda nyumbani kwake kumuona muda huu.”

“Tangu kutekwa kwa Mo nimekuwa karibu sana na familia yake katika kipindi chote hicho kwani nilikuwa nawatembelea. Lakini mimi ni mtu wa karibu sana wa Mo na tumejuana zaidi ya miaka kumi,” amesema Makamba.

“Kwa hiyo alipopatikana baba yake (Gullam) alinipigia simu na kuniambia kuna jambo la furaha kwamba Mo amepatikana akampa simu nikazungumza naye. Wakati huo ilikuwa saa 9.09 usiku.”

Amesisitiza, “Kwa kuwa hapa ninapoishi si mbali na anapoishi  Mo ni kama umbali wa dakika tano hivi, nikasema siwezi kulala acha niende kumuona. Nilipofika  ilikuwa furaha sana na tulikumbatiana na tukazungumza.”

Amesema wakati anakwenda kumwona Mo hata polisi walikuwa hawajafika nyumbani hapo.