Naibu waziri wa zamani asema amefika kituoni

Muktasari:

  • Amemkabidhi kijiti mrithi wake aendelee na safari ya kuwatumikia Watanzania.

Dodoma. Aliyekuwa Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Anastazia Wambura ameufananisha utumishi wa umma na chombo cha usafiri ambacho abiria hushuka kituoni baada ya kufika na dereva kuendelea na safari.

“Mheshimiwa waziri, viongozi wenzangu na ndugu zangu watumishi wa wizara, mimi nimefika kituoni, naibu waziri nakukabidhi kijiti endelea na safari, endelea kuwatumikia Watanzania kama ambavyo ilani ya chama tawala inavyoeleza,” amesema Wambura.

Amesema hayo leo Jumanne, Oktoba 17,2017 baada ya mrithi wake Juliana Shonza kuwasili katika ofisi za wizara mjini Dodoma na kupokewa na Waziri wa wizara hiyo, Dk Harrison Mwakyembe, viongozi wa wizara na watumishi wengine.

Wambura amempongeza Shonza kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo. Pia, amemshukuru Rais John Magufuli kwa kumuamini na kumpa nafasi ya kuwatumikia Watanzania.

Kwa upande wake, Shonza ameahidi kushirikiana na watendaji wa wizara, wadau na wananchi kwa jumla kusimamia maadili ya Mtanzania.

“Wizara hii ni muhimu kwa kuwa inajenga taswira ya Taifa kupitia sekta zake za habari, utamaduni, sanaa na michezo hivyo nitahakikisha tunashirikiana kwa karibu katika kuwatumikia wananchi,” amesema Shonza.

Amesema atahakikisha maadili bora kwa jamii yanazingatiwa ili kuendelea kujenga Taifa imara kwa kuzingatia mavazi yenye heshima na nyimbo zenye kujenga.

Shonza katika taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari (Maelezo) amesema ni wajibu wao wakiwa watumishi wa umma kuhakikisha wanatekeleza ilani ya chama tawala kilichoahidi kuwatumikia Watanzania ili kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa kwa wakati.

Waziri Mwakyembe amemuahidi ushirikiano wa hali na mali Shonza katika kuwahudumia wananchi kupitia sekta za habari, utamaduni, sanaa na michezo.