Aliyeishi kwa kutegemea mafuta, sukari sasa ni mwendo wa nyama, wali, ugali

Muktasari:

Badala ya kutegemea mafuta, sukari na maziwa, sasa mwili wa Shukuru (16) hauhitaji vitu hivyo bali anakula wali, mayai, uji, ugali na mbogamboga.

Dar es Salaam. Afya ya Shukuru Kisonga, aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa usiofahamika na kumsababishia kuishi kwa kula sukari, mafuta ya kula na maziwa imezidi kuimarika na sasa ameanza kusahau mlo huo wa ajabu.

Badala ya kutegemea mafuta, sukari na maziwa, sasa mwili wa Shukuru (16) hauhitaji vitu hivyo bali anakula wali, mayai, uji, ugali na mbogamboga.

Akizungumza na gazeti hili jana, mama mzazi wa kijana huyo Mwanahabibi Mtenje aliwashukuru Watanzania na uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa kuwa mwanaye anakula kila kitu tofauti na alivyofikishwa hospitalini hapo. “Sasa hivi anakula kila kitu hadi nashangaa kwa kweli.Anakula ndizi za kukaanga, mayai, wali pia anakunywa uji na soda.Ni Jambo la kumshukuru Mungu kwa hatua hii aliyofikia Shukuru,” alisema Mwanahabibi.

Mzazi huyo alisema hana neno la kusema zaidi ya kuwashukuru Watanzania, uongozi wa Muhimbili na waandishi wa habari kwa namna walivyomsaidia Shukuru kufikia hatua hiyo.

Shukuru alilazwa wiki iliyopita katika hospitali hiyo kutokana na ugonjwa huo ambao baada ya kuchukuliwa vipimo aligundulika kuwa na tatizo na Selimundu (sickle cell). Kwa mujibu wa mama huyo kabla ya kufikishwa Muhimbili, kijana huyo akikosa kula mafuta, maziwa na kubwia sukari ilikuwa ni sawa na gari lililoisha mafuta.

Hata hivyo, Mei 23 akitoa majibu ya vipimo vya Shukuru, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu Muhimbili, Stella Rwezaura alisema mganga wa kienyeji ndiye aliyetoa ushauri wa kumpa vyakula hivyo mtoto huyo ili kumpa ahueni bila kujua anasumbuliwa na kitu gani.

Dk Stella alisema katika uchunguzi wao walibaini kuwa alikosa madini ya chuma yaliyomsababishia mwili wake kutamani kula mafuta, sukari na maziwa. Hata hivyo ameshaanza dawa za matibabu.

Kwa upande wake, Shukuru alisema, “Sijambo namshukuru Mungu. Sasa naagiza chakula chochote nitakachohitaji.”

Meneja Uhusiano wa Muhimbili, Aminiel Aligaesha aliungana na Mwanahabibi na kusema afya ya Shukuru inazidi kuimarika siku hadi siku na kwamba, hivi sasa anakula vyakula mbalimbali.

Alipoulizwa kuhusu kutoka hospitalini hapo alijibu; “ Siwezi kujua ataruhusiwa lini ila madaktari ndio watakuwa na majibu zaidi baada ya kuridhika na afya yake.”