VIDEO: Aliyekuwa anaendesha kivuko ni ‘deiwaka’

Muktasari:

Rais Magufuli amelihutubia Taifa akizungumzia masuala kadhaa yaliyojitokeza katika ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere na amesema kutakuwa na siku nne za maombolezo kuanzia leo Ijumaa na bendera zitapepea nusu mlingoti, lakini imebainika kuwa aliyekuwa anaendesha kivuko hicho hakuwa nahodha mwenyewe.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amezungumzia ajali ya Kivuko cha Mv Nyerere akidokeza mambo yaliyosababisha kutokea kwa ajali hiyo kuwa ni pamoja na nahodha wa kivuko hicho kuwa si mwenyewe ila ‘deiwaka’.

Rais Magufuli akihutubia Taifa kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC1) saa 1 usiku leo Ijumaa, ametoa pole kwa ndugu na Watanzania kufuatia ajali hiyo iliyotolea jana Alhamisi mchana na kuua watu 136.

Amesema kivuko hicho kina uwezo wa kubeba watu 100 au 101 lakini ilibeba watu zaidi, “Taarifa za awali, tulizopata kutoka kwa mashuhuda, Kivuko hicho mpaka sasa hivi (saa 1.14 jioni) maiti 131 na majeruhi 40, tayari imefika 171 na maiti bado wako.”

Amesema kuna taarifa kuwa kivuko kilikuwa kimepakia mahindi mengi tu, bia na soda, ilipakia vifaa mbalimbali.

“Hata aliyekuwa anaendesha hiyo feri, siyo nahodha mwenyewe, yeye hakusafiri na inadaiwa amekamatwa na wote wakamatwe,” amesema huku akisisitiza uchunguzi ufanyike na hatua za kisheria zichukuliwe kwa wale wote waliohusika

Rais Magufuli amesema tayari Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Hussein Mwinyi, vyombo vya ulinzi na usalama  kama Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), jeshi la wana maji, Polisi, Sumatra na kamati ya ulinzi na usalama ya Mwanza, Kamati ya maafa ya ofisi ya waziri mkuu, “Wako kule wanaendelea na operesheni ya kutoa miili iliyonasa ndani ya kivuko.”

Katika hotuba yake ya chini ya dakika kumi, Rais Magufuli amewataka wanasiasa kutokutumia msiba huo kisiasa, “Tuviache vyombo vinavyohusika na uchunguzi, vifanye kazi yake, vifanye uchunguzi vitatoa taarifa.”

“Wale watakaobainika watafikishwa mahakamani na vifo vya Watanzania tusivitumie kisiasa, vyombo vyenye utaalamu vitatoa taarifa yake,” ameongeza: