Aliyekuwa kigogo wa FFU na wenzake saba watupwa jela kwa wizi wa SMG

Muktasari:

Bhoke Bruno na wenzake saba jana Jumatano walihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la kuiba bunduki nane aina ya SMG, mali ya mwajiri wao.

Tabora. Aliyekuwa Mkuu wa Kikosi cha Polisi cha Kutuliza Ghasia (FFU), Mkoa wa Tabora, Mrakibu Msaidizi wa Polisi, Bhoke Bruno na wenzake saba jana Jumatano walihukumiwa kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la kuiba bunduki nane aina ya SMG, mali ya mwajiri wao.

Wengine waliohukumiwa kifungo katika hukumu iliyosomwa na Kaimu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora, Sharmira Sarwatt ni Koplo Idd Abdalah, PC Mwinyi Gonga na Said Mgonela, wote kutoka kikosi cha FFU Tabora.

Kwa pamoja, waliokuwa waajiriwa hao wa jeshi la polisi kwa pamoja walitiwa hatiani kwa makosa matatu ya kula njama, kuiba na kushindwa kuzuia tukio.

Mahakama pia iliwapa adhabu kama hiyo washtakiwa wengine watatu Shaban Haruna, Shaban Kabanika na Idd Supu waliodaiwa kushirikiana na waliokuwa maofisa hao wa polisi.

Washitakiwa wengine watatu kati ya 10 waliokuwa wakishtakiwa, Charles Abihud, Emmanuel Festo na Nicholaus Mlelwa, waliachiwa huru baada ya ushahidi dhidi yao kukosekana.

“Ushaihidi uliowasilishwa na upande wa Jamhuri umeithibitishia Mahakama pasipo shaka kuwa washtakiwa saba kati ya 10 walihusika na makosa yanayowakabili, hivyo wanahukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kila kosa,” alisema Sarwatt.

Kutokana na adhabu ya makosa yote matatu yanaenda pamoja, washtakiwa watakaa magereza kwa miaka mitano.

Awali upande wa mashtaka ulioongozwa na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Juma Masanja uliiambia Mahakama kuwa kwa pamoja, wahtakiwa walitenda makosa hayo kati ya Aprili 2013 hadi Aprili 2014.

Katika shtaka la kwanza, ilidaiwa kuwa washtakiwa kwa nyakati tofauti, walikula njama ya kuiba bunduki aina ya SMG zilizokuwa zikihifadhiwa katika ghala la kituo cha FFU mjini Tabora.

Upande wa mashitaka ulidai katika shitaka la pili kuwa katika kipindi hicho washitakiwa kwa pamoja washtakiwa bila kuwa na uhalali, walichukua bunduki nane kwenye ghala hilo, wakati shtaka la tatu likiwa ni kushindwa kuzuia uhalifu kutendeka ambalo.

Katika shauri hilo la jinai namba 104/2015, washtakiwa waliwakilishwa na mawakili Kelvin Kayaga na Mussa Kassimu wa mjini Tabora.