Aliyekuwa mhasibu Takukuru, wenzake wafikishwa kortini

Muktasari:

Wakabiliwa na mashtaka 43 likiwamo la kumiliki mali ambazo hazina maelezo yake

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mhasibu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Godfrey Gugai amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na wenzake watatu wakikabiliwa na mashtaka 43 likiwamo la kumiliki mali ambazo hazina maelezo zenye thamani ya Sh3.6 bilioni.

Akisoma hati ya mashtaka jana kwa Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Wakili wa Serikali, Wankyo Simon aliwataja washtakiwa wengine kuwa ni George Makaranga, Leonard Alloys na Yasini Katera.

Washtakiwa hao, pia wanakabiliwa na mashtaka 22 ya kughushi na 20 ya utakatishaji wa fedha.

Wakili Simon alidai kati ya Januari na Juni, 2016 Dar es Salaam, Gugai akishirikiana na wenzake walighushi mikataba ya mauziano akionesha ameuza mali zake kwa wenzake na watu wengine wakati akijua siyo kweli.

Alidai kuwa Gugai anadaiwa Agosti 14, 2009 alighushi mkataba wa mauziano akionesha amemuuzia Zena Mgallah, ploti namba 225, block 6 Mbweni JKT, wakati akijua siyo kweli.

Alidai Julai 5, 2011 alighushi mkataba kumuuzia Salehe Sas ploti namba 621,622 na 623 block A zilizopo Gomba Arumeru.

Wakili Wankyo alidai kuwa Oktoba 20, 2013 alighushi mkataba akionesha kumuuzia Arif Premji ploti namba 64 eneo la Onunio Kinondoni.

Desemba 20, 2014 alighushi mkataba akionesha kumuuzia Edith Mbatia ploti namba 737 block C, iliyopo Mwambani Mwarongo Tanga na ploti namba 1, 2 na 3.

Alidai kuwa Novemba 20, 2009, washtakiwa hao waligushi kuonesha Gugai alimuuzia Makaranga ploti namba 150 block 8 ya Bunju Kinondoni.

Wakili Simon alidai kuwa Novemba 19, 2009, walighushi mkataba wakionesha Gugai alimuuzia Alloys ploti namba 275, 277, 296 na 297 block 2 zilizopo Nyamongo, Mwanza.

Hata hivyo, washtakiwa hao walikana mashtaka hayo.

Mawakili wa utetezi, Alex Mgongolwa na Semi Malimi walidai kuwa shtaka la 23 hadi 43 ya utakatishaji fedha hayakidhi vigezo vinavyotakiwa kwa makosa ya utakatishaji wa fedha.

Mgongolwa alidai kwa kuwa makosa hayo hayaelezi kosa husika, aliomba Mahakama iyafutilie mbali chini ya kifungu cha 129 cha makosa ya jinai.

Alidai kuwa katika mashtaka yanayowakabili wateja wake hayazungumzii fedha ambayo ndiyo msingi wa shtaka la utakatishaji fedha na kwamba katika kesi hiyo kinachojitokeza ni kwamba alidanganya mali ya fulani wakati siyo.