Ally Saleh: Zanzibar salama inategemea usalama wa CUF

Mbunge wa Malindi, Ally Saleh

Muktasari:

  • Kwa takriban mwaka mmoja sasa, CUF iko kwenye mgogoro baada ya mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu nafasi hiyo na baadaye kutengua, hatua ambayo ilipingwa na wajumbe wa mkutano mkuu wanaomuunga mkono katibu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Dar es Salaam. Wakati CUF ikiendelea kukabiliana na mgogoro, mbunge wa Malindi, Ally Saleh amesema chama hicho hakiwezi kukubali kuvurugwa kwa kuwa usalama wake ndio usalama wa Zanzibar.

Kwa takriban mwaka mmoja sasa, CUF iko kwenye mgogoro baada ya mwenyekiti wake, Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu nafasi hiyo na baadaye kutengua, hatua ambayo ilipingwa na wajumbe wa mkutano mkuu wanaomuunga mkono katibu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Akizungumza na gazeti hili katika mahojiano maalumu (yamechapishwa Ukurasa 23 na 24 wa gazeti hili), Saleh alisema juhudi zozote zinazofanywa ili kuivuruga CUF zitakuwa na athari kubwa kwa upande wa Zanzibar kwa kuwa chama hicho na CCM ndivyo vyenye wafuasi wengi.

“Zanzibar ni nusu kwa nusu, hawa wanaochochea matatizo lazima watambue athari zake. Ukiivuruga CUF, ikitokea matatizo utamuita nani kuzungumza naye? alihoji Saleh ambaye pia ni Naibu Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

“Hatupendi kuona haya yanayoendelea kwenye chama chetu, ndiyo maana hadi sasa tumefungua kesi 13 ili kuzuia njama zozote za kuiangamiza CUF. Nje ya mahakama mchezo huu unachezwa na CCM kwa kushirikiana na dola,” alidai Saleh ambaye pia ni mwanasheria.

Akitoa maoni yake kuhusu siasa za Tanzania tangu ulipomalizika Uchaguzi Mkuu 2015, Saleh alisema Taifa linapita katika kipindi kigumu kutokana na viongozi kutokubali kushaurika. “Tuna viongozi wanaotaka kutengeneza utambulisho wao kwa kufuta yote yaliyofanywa na viongozi waliopita. Tanzania haikuanza leo haiwezekani kuongoza bila kuangalia mambo ya nyuma. Matokeo ya staili hii ya uongozi hayataifikisha mbali Tanzania,” alisema Saleh.

Tangu ilipoingia madarakani Novemba, 2015, Serikali ya Awamu ya Tano imezuia mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa na kuzuia mijadala ya bungeni kurushwa moja kwa moja na vituo vya televisheni.

Saleh alisema licha ya kuamini kazi anayofanya Rais Magufuli, hakubaliani na uamuzi wa Serikali yake unaoonekana kuwazuia wananchi kutoa maoni yao.

“Tusikatazane kutoa maoni. Rais aone tunachokisema ni kwa ajili ya wema wa nchi hii. Unapokuwa na nchi inayosema kupitia mijadala, midahalo na makongamano unakuwa na nchi nzuri. Wanaomshauri Rais wamwambie kuwa wanaotoa maoni yao wanalitakia mema Taifa,” alisema Saleh.

Saleh pia alitaja mambo mawili yanayomuweka katika wakati mgumu tangu alipochaguliwa, kuwa ni pamoja na Muungano na wabunge kutanguliza vyama katika mambo yanayohusu mustakabali wa Taifa.

“Wazanzibari wengi walitaka nizungumzie Muungano, lakini tunapojaribu kufanya hivyo bungeni wanatuzuia. Pia, kuna wakati mnakaa kwenye kamati na kufanya uamuzi, lakini mkiwa bungeni wanaamua kwa masilahi ya vyama na si Taifa,” alisema kiongozi huyo ambaye ni mjumbe wa Kamati ya Sheria ya Bunge.

Uchaguzi 2019/20

Saleh pia alibainisha kuwa itakuwa vigumu kujipanga kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na Uchaguzi Mkuu 2020 kama wataendelea kukabiliwa na mgogoro.

“Ndio maana tunakwenda mahakamani, hatutaenda barabarani,” alisema.

Mhitimu huyo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia alizungumzia wajibu wa vyuo vikuu katika kuandaa vijana watakaokuwa na uzalendo kwa Taifa kama ilivyokuwa zamani.“Sisi tulijitambulisha kama vijana wa Taifa na si vijana wa vyama, kuna mahali tumekosea kama Taifa. Ni muhimu vyama vya siasa kupika makada wake chuoni lakini jambo la muhimu zaidi ni Tanzania,” alisema.