Amri ya JPM ilivyowaponza wamachinga Mwanza

Askari polisi wakiwa wametanda katika mitaa ya Jiji la Mwanza baada ya kuwatawanya machinga waliokuwa wanapanga bidhaa zao kwenye barabara mbalimbali. Picha na Michael Jamson

Muktasari:

Sisi tutatetea haki na masilahi ya machinga ya kuwapo maeneo ya katikati ya mji yanayofikika kirahisi na palipo na wateja pia, lakini siyo uvunjifu wa sheria kwa kupanga bidhaa barabarani na kwenye njia za waenda kwa miguu.”

Wiki iliyopita tulishuhudia sakata la machinga na uongozi wa Jiji la Mwanza ukiibuka upya licha ya kuwapo amri ya Rais John Magufuli ya kuzuia wafanyabiashara hao wadogo kuhamishwa bila majadiliano wala kutengewa maeneo maalumu.

Februari 17, 2017 mgambo wa jiji walikabiliana na machinga katika operesheni ya kuwaondoa wale waliotandaza bidhaa zao barabarani na kwenye njia za waenda kwa miguu jirani na Msikiti wa Swaminarayan, eneo la Makoroboi.

Eneo la Makoroboi ni uchochoro maarufu kwa biashara ndogondogo jijini Mwanza uliopo pembezoni mwa miamba ya mawe inayolipamba jiji hilo. Kama lilivyo jina lake, kwa miaka mingi uchochoro huo ulitawaliwa na mafundi wengi wanaotengeneza vibatari (makoroboi) kabla ya kuvamiwa na machinga.

Mapambano kati ya makundi haya mawili yaliyozoeleka katika maeneo mbalimbali nchini yamekuja miezi kadhaa baada ya amri ya Rais Magufuli ya kutengua operesheni ya kuwaondoa katikati ya Jiji la Mwanza iliyofanyika Desemba 3 na 4, mwaka jana.

Chini ya Sheria ya Mipango Miji Sura namba 8 ya mwaka 2007 na ile ya Mazingira namba 25 ya mwaka 1972, jiji liliwaondoa machinga katikati ya jiji kwa gharama ya zaidi ya Sh200 milioni, fedha zilizotumika kujaza mafuta kwenye magari na posho mbalimbali za watekelezaji.

Hata hivyo, Rais Magufuli alitengua operesheni hiyo akiwalaumu viongozi wa jiji kwa kuwahamisha machinga bila kuwatengea maeneo mapya wala kufanya majadiliano nao.

Uamuzi wa Rais Magufuli ulisababisha viongozi wa Serikali na Jiji la Mwanza kupigwa ganzi na kuacha kuwadhibiti machinga wakitumia vibaya amri hiyo kutandaza bidhaa za kila eneo waliloona liko wazi.

Huo ndiyo ulikuwa mwanzo wa baadhi ya barabara yakiwamo makutano ya Barabara za Nyerere na Pamba kufungwa na machinga waliotandaza bidhaa zao kiasi cha magari kushindwa kupita.

Kila mahali, kuanzia njia za waenda kwa miguu, vichochoro na viambaza vya maduka kote kulipangwa bidhaa za machinga.

Wakati machinga ni kete muhimu kisiasa kutokana na viongozi wanaochaguliwa kwa kura kuwakingia kifua dhidi ya uamuzi wa watendaji unaosimamia sheria, ni dhahiri wafanyabiashara hao wa Mwanza walitumia vibaya amri ya Rais ya kuwarejesha katikati ya jiji.

Tangu warejeshwe, machinga wamekuwa na tabia ya kiburi, dharau na hata kauli za kebehi dhidi ya viongozi wa jiji na Serikali kwa kuwatishia kuripoti kwa Rais kila wanapotakiwa kuzingatia sheria katika shughuli zao.

Yawezekana ni hofu, mshtuko au kususa. Lakini viongozi na watendaji jijini Mwanza walionyesha udhaifu kwa kuwaachia machinga kutamba kwa kupanga bidhaa barabarani na kwenye njia za waenda kwa miguu kwa takriban miezi miwili tangu Rais atengue operesheni yao.

Tangazo la hivi karibuni la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene la kuwaagiza viongozi wa halmashauri zote nchini kudhibiti biashara holela kwenye maeneo yasiyoruhusiwa ndilo limewapa nguvu na kuwashtua kuanza kusimamia sheria.

Baada ya tangazo hilo, Februari 6, mwaka huu jiji nalo lilitoa siku tatu machinga kuondoa bidhaa zao barabarani na kwenye njia za waenda kwa miguu kabla au ifikapo Februari 9, mwaka huu.

Kwa kutumia sheria ndogo za usafi wa mazingira za Halmashauri ya Jiji la Mwanza za mwaka 2010 na kanuni za Serikali za Mitaa na Mamlaka za Miji za uendeshaji wa miji za mwaka 2008, jiji likaendesha operesheni mpya ya kuwaondoa wafanyabiashara hao kutoka maeneo yasiyoruhusiwa.

Lakini safari hii, ingawa kumekuwapo vitendo vya kutumia nguvu kupita kiasi, wamewaelekeza wote waende kwenye maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili yao.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa Jiji la Mwanza, Kiomoni Kibamba maeneo rasmi yaliyotengwa ni Makoroboi, Mlango Mmoja, Asante  Moto, Tanganyika, Sahara, Dampo, Market  Sreet, Nyegezi, Buzuruga, Mirongo na Liberty.

“Wanaoendesha shughuli zao nje ya maeneo hayo tutawaondoa kwa sababu wanakiuka sheria, taratibu na makubaliano kati ya mamlaka za Serikali na viongozi wa wamachinga,” anasema Kibamba.

Tofauti na operesheni ya awali, safari hii hata Mwenyekiti wa Shirika la Umoja wa Machinga Mwanza (Shiuma), Matondo Masanja anaunga mkono uamuzi kuwaondoa wafanyabiashara wanaotandaza bidhaa barabarani na kwenye njia za waenda kwa miguu.

“Sisi tutatetea haki na masilahi ya machinga ya kuwapo maeneo ya katikati ya mji yanayofikika kirahisi na palipo na wateja pia, lakini siyo uvunjifu wa sheria kwa kupanga bidhaa barabarani na kwenye njia za waenda kwa miguu,” anasema Masanja.

Mwenyekiti huyo wa Shiuma anawataka machinga wote jijini Mwanza kuendesha shughuli zao katika maeneo kumi maalumu yaliyotengwa kwa ajili yao.

“Maeneo tuliyokubaliana na jiji ni Makoroboi, Mlango Mmoja, Asante  Moto, Tanganyika, Sahara, Dampo, Market  Sreet, Nyegezi, Buzuruga, Mirongo na Liberty, wanaokuwa nje ya hapo wanakiuka sheria na hatutawatetea,” anasisitiza Masanja.

Meya wa Jiji la Mwanza, James Bwire anasema jiji litaendelea kuzingatia sheria, kanuni na taratibu katika kusimamia shughuli zote ikiwamo biashara ya machinga.

“Wakati jiji tukiendelea kutekeleza agizo la Rais kwa kuandaa maeneo na miundombinu bora ya kibiashara, machinga lazima waheshimu sheria, kanuni na taratibu za nchi pamoja na sheria ndogo za halmashauri za jiji,” anasisitiza Bwire.

Tatizo la wanasiasa

Ni kweli kwamba machinga ni wapigakura kama yalivyo makundi mengine. Lakini hilo haliwapi haki ya kukiuka sheria, kanuni na taratibu kwa kiburi cha kulindwa na wanasiasa.

Historia inaonyesha kuwa kila mgogoro kati ya mamlaka za miji na machinga inapoibuka, wanasiasa mara nyingi husimama upande wa wafanyabiashara hao.

Mbunge wa sasa wa Nyamagana, Stanslaus Mabula na hata mtangulizi wake, Ezekiah Wenje ni kati ya wanasiasa wanaotangaza hadharani kuwaunga mkono machinga, hata pale wanapokiuka sheria kutokana na masilahi ya kisiasa.

Katika mkutano wake wa hadhara eneo la Igoma, Mabula siyo tu aliwaunga mkono kurejeshwa katikati ya mji, bali pia alijitolea kuwalipia gharama za mawakili kwa ajili ya kudai mali zao zilizoharibika wakati wa operesheni ya Desemba 3 na 4, mwaka jana.

Kuna ugumu kiutendaji kwa viongozi wa halmashauri kutokana na rungu la wanasiasa katika usimamizi wa sheria, lakini hilo halistahili kuwazuia kusimamia na kutekeleza sheria ya mipango miji.

Yawezekana viongozi wa mkoa na Jiji la Mwanza walifanya makosa katika utekelezaji wa operesheni ya awali ikiwamo madai ya kutoshirikisha wadau wote katika utekelezaji wa mpango huo, lakini ni vema wanasiasa wakaacha kuingilia na kutengua masuala yanayofanyika kwa kuzingatia sheria likiwemo hili la machinga.

Hatuwezi kuwa na jamii bora iwapo tutaruhusu mambo kufanyika kiholela kama tunavyoshuhudia kwenye miji yetu. Shughuli zote sharti zifanyike kwa mujibu na misingi ya sheria hata kama kwa kufanya hivyo wapo wachache watakaoumia.

Ni ukweli usiopingika kuwa idadi ya machinga inaongezeka kila siku na hivyo kuzidi uwezo wa maeneo wanayotengewa kwa ajili yao, lakini hiyo isiwe kigezo wala sababu ya kuruhusu biashara holela mitaani.

Hatuwezi kugeuza kila eneo la wazi, barabara na njia za waenda kwa miguu kuwa masoko ya machinga. Hili haliwezekani kamwe.

Lazima tujiwekee na kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za mipango miji, ili siyo tu kufanya miji yetu kuwa nadhifu, bali pia kurahisisha utoaji wa huduma zingine za kijamii kwa makundi yote.

Viongozi wa Serikali za mitaa wasinyong’onyee mbele ya machinga kwa kuhofia rungu la Rais, bali wazingatie maelekezo ya kiongozi huyo kwa kushirikiana na wafanyabiasha hao na  wadau wengine kutafuta maeneo rafiki na yenye miundombinu ya kuwahamishia.

Shughuli za kujitafutia riziki, ikiwamo umachinga zifanyike kwa kuheshimu sheria, kanuni na taratibu bila kuelemewa na matamanio ya kisiasa kuelekea Uchaguzi Mkuu ujao wa 2020.