Anayetaka kujiua atajichoma sindano yenye dawa

Muktasari:

Tayari mtu huyo amechangia Dola 20,000 ili akamilishe azma yake hiyo

Habari ya mwanasayansi David Goodall anayetarajiwa kuchomwa sindano ya sumu kesho imevutia hisia za watu wengi duniani, tofauti na wengi waliowahi kufikia hatua hiyo, huku ikielezwa kuwa atajichoma mwenyewe sindano yenye dawa itakayosababisha afariki dunia.

Goodall ambaye kesho atahitimisha safari yake duniani, anasema anaisubiri dakika ambayo atashika bomba la sindano na kubonyeza sumu ndani ya mwili wake.

Akizungumza na kituo cha CNN nchini Uswisi huku akihesabu saa za kuifikia hatua hiyo, anasema anaamini litakuwa tendo la faraja kwake kujisukumia dawa aina ya sodium pentobarbital katika mshipa wake.

“Naamini kitakuwa kifo kizuri na ni wakati ambao nausubiri kwa hamu,” anasema Goodall akiwa katika kitanda cha hospitali mjini Basel nchini humo.

Madaktari wanne Sheena McKenzie, Melissa Bell, Saskya Vandoorne na Ben Westcott watamsaidia hatua za awali katika kuweka dawa na kuchomeka sindano katika mshipa, naye atabakiwa na kazi moja tu ya kusukuma dawa.

Goodall mwenye umri wa miaka 104 raia wa Australia aliomba kufa kwa hiyari kwa madai ya kuchoshwa na maisha. Hata hivyo, hakuruhusiwa kufanya hivyo nchini kwake na kulazimika kusafiri mpaka Uswisi kuhitimisha safari yake duniani.

Wasamaria wema walimchangia kiasi cha dola 20,000 ambazo ni wastani wa Sh45 milioni ili kukamilisha azma yake hiyo.