Aneth Kushaba afunguka kuimba injili, maisha ya kuongoza bendi

Aneth Kushaba


Muktasari:

Alijiunga na Bendi ya Skylight, iliyozidi kumuongezea umaarufu 

Dar es salaam. Aneth Kushaba ni jina ambalo lilianza kufahamika vyema kwa wapenzi wa burudani kuanzia katika shindano la kusaka na kuibua vipaji, linalojulikana kama Tusker Project Fame (TPF), linalohusisha waimbaji mbalimbali kutoka Afrika Mashariki.

Mwaka 2010, Davies Sondela kutoka Rwanda ndiye aliyeibuka mshindi namba moja, namba mbili ilienda kwa Mtanzania Peter Msechu ambaye alionesha umahiri mkubwa sana na kujizolea mashabiki wengi hasa kutokana na vituko alivyokuwa anavifanya kama moja ya kunogesha mashindano hayo.

Kwa upande wake, Aneth alikamata nafasi ya tisa katika shindano hilo, lakini kwake tayari alikuwa amepata mashabiki wa kutosha hasa kutokana na ucheshi wake kipindi chote cha shindano hilo pamoja na staili yake ya uimbaji.

“Aisee kushiriki shindano lile ilikuwa ni ndoto yangu kubwa, ingawa nilikuwa naimba kabla ya hapo ila nilikuwa sijulikani, hivyo Tusker Project Fame ilikuwa njia rasmi ya kunionyesha kwa watu kujua kipaji changu,” anasema.

Baada Ya Tusker?

Alijiunga na Bendi ya Skylight, iliyozidi kumuongezea umaarufu kutokana na namna ambavyo anajua kuipangilia sauti anapoimba inakuwa nyororo na kusababisha mashabiki kuvutiwa kumsikiliza anapokuwa jukwaani.

Kushaba anasema ameanzisha bendi inayojulikana kwa jina la Star na anaeleza namna anavyoweza kupiga pesa kwa nyakati zote, akisema yeye ni msanii pekee anayechukua kiasi kidogo anapoalikwa kwenye matamasha ya kuimba.

“Bendi inakuwa na watu 12, kwa maana ya wapiga gitaa, drums, waimbaji na wale wanaocheza, lakini ikitokea ofa imekuja ni ya watu sita basi naenda na idadi hiyo na kama kuna wale wa kima cha chini kabisa naenda na watatu.

“Napata kipato kinachoendana na kazi yangu, mimi sio kama mabinti ambao wanajiweka wa gharama wakati hawana kitu na mwisho wake wanaishi maisha ya kuigiza ambayo hayana uhalisia,” anasema.

Ukiachana na bendi, aliweza kuachia ngoma kadhaa kama ‘Siku nazo’ na ‘I like it’ ambazo zilifanya vyema sokoni na kupigwa katika vituo mbalimbali vya redio. Kushaba ameenda mbali licha ya kuimba muziki wa kidunia, lakini pia amekuja na kitu kipya kwa kuimba nyimbo za dini na tayari ameishatoa kibao kinachojulikana kama ‘Haleluya’.

Alipoulizwa amepokelewaje sokoni kutokana na kuimba nyimbo za kidunia na dini, anasema, “hii si kwa mashabiki tu hata wachungaji wapo wanaoelewa na wasionielewa kabisa, ila wafahamu kuwa ninapokuwa na bendi ni kazi inayonipa kipato, lakini injili ninamtukuza Mungu wangu kwa imani yangu.

“Kama Mungu angekuwa hapendi sidhani kama ningepata pesa za kuwalipa mishahara watu kwenye bendi yangu ya Star, ni kweli naimba nyimbo za mapenzi lakini siingii ndani zaidi naimba. Nyimbo nazopenda ni za kina R Kelly, Mariah Carey, lakini kwa hapa nyumbani nawapenda Fid Q, Paul Clement na Diamond Platnumz,” anasema.