Anglikana kwachemka, Askofu Mokiwa aamriwa kujiuzulu

ASKOFU MOKIWA

Dodoma. Mgogoro umeibuka katika Kanisa la Anglikana Jimbo Kuu la Tanzania baada ya kumuamuru Askofu wa kanisa hilo Dayosisi ya Dar es Salaam, Dk Valentino Mokiwa kujiuzulu na kustaafu kwa lazima kwa kile kinachoelezwa kuwa amesigina katiba ya kanisa.

Taarifa zilizopatikana jana na kusambaa kwenye mitandao ya kijamii, zilionyesha barua iliyoandikwa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo, Dk Jakob Chimeledya kumtaka Mokiwa ajiuzulu wadhifa huo na kuliacha kanisa chini ya uangalizi wake.

Jana, Askofu Chimeledya alithibitisha kuandika barua hiyo lakini akasema hawezi kusema zaidi kwa kuwa anasubiri utekelezaji wa maagizo yake.

“Nimeandika barua mbili. Hiyo ya kumtaka Askofu ajiuzulu niliandika mimi na niliagiza isomwe kwenye makanisa yote ya Dayosisi ya Dar es Salaam leo (Jana), sababu zipo ndani ya barua,” alisema Dk Chimeledya.

Askofu Mokiwa ambaye ndiye aliyemwachia Dk Chimeledya uaskofu mkuu wa kanisa hilo, aliingia kwenye mgogoro na waumini wake mapema 2015 wakimtuhumu kutumia vibaya madaraka yake na kufuja mali za kanisa, huku akifanya mipango ya kuitenga dayosisi yake na kanisa kwa ngazi ya jimbo.

Waumini walipeleka mashtaka kwa Askofu Mkuu Machi 2, 2015 wakimtuhumu Mokiwa kwa ukosefu wa maadili kwa mujibu wa kifungu cha 17(2) na hivyo kutoa mapendekezo ya kunyang’anywa madaraka yake.

Katika barua ya Askofu Chimeledya yenye kurasa 14,  ametaja mambo 10 yaliyofanya uongozi ufikie uamuzi wa kumstaafisha Mokiwa, ambayo hata hivyo alipoulizwa na gazeti hili aliyakana yote.

Miongoni mwa tuhuma hizo ni pamoja na kuhamasisha dayosisi yake kujitenga katika udhamini wa Anglikana, kufuja mali za kanisa kwa kuingia mikataba mibovu, kushindwa kutatua migogoyo ya makanisa katika baadhi ya mitaa na migogoro ya waumini na mapadri.