Anne Makinda apata mrithi TBT

Muktasari:

Ni kufuatia Rais John Magufuli kuteua mtu wa kuchukua nafasi yake


Dar es Salaam. Rais John Magufuli amemteua mhandisi Steven Mlote kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Chai Tanzania (TBT) kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Spika wa zamani wa Bunge, Anne Makinda ambaye amemaliza muda wake.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Mei 23, 2018 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa  imemkariri Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi kuwa uteuzi wa Mlote umeanza juzi Mei 21, 2018.

Inaeleza kuwa kiongozi mkuu huyo wa nchi pia amemteua Geofrey Mkamilo kuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI).

Inafafanua kuwa uteuzi wa Dk Mkamilo umeanza Mei 22, 2018. Kabla ya uteuzi huo Dk Mkamilo alikuwa mkurugenzi wa utafiti wa kilimo, kanda ya mashariki, kituo cha utafiti wa kilimo cha Ilonga Mkoa wa Morogoro na amechukua nafasi na Dk Fidelis Myaka ambaye amestaafu.